Breaking News
Loading...

Advert

Friday, May 13, 2016

Washiriki wa mkutano wa kimataifa wavutiwa na tanzania jinsi inavyopambana na rushwa.soma zaid.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema viongozi
wakuu wa nchini na washiriki wa mkutano wa
kimataifa wa kupambana na rushwa wamevutiwa
na jitihada ambazo Tanzania imezichukua
kukabiliana na janga hilo.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Mei 13, 2016)
wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake
kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa
Nchi ulioitishwa kujadili suala la kupambana na
rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini
London, Uingereza.
Waziri Mkuu alisema katika kikao cha kwanza
kilichohudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi
wa kitaifa wapatao 20, alipata fursa ya kuelezea
jinsi Tanzania ilivyoweza kupambana na rushwa
kwa kuzingatia vigezo vikuu vinne.
Waziri Mkuu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni
kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria
zinazohusu masuala ya rushwa; uanzishwaji wa
mahakama maalum ya mafisadi ambayo
inatarajiwa kuanza kazi Julai, mwaka huu;
mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya
wananchi na utaratibu wa kubaini wala rushwa
kwa kushirikisha jamii ikiwemo kutunza siri za
watoa taarifa.
“Ziko sheria ambazo zinafanyiwa kazi hivi sasa
ambazo ni lazima zipitishwe na Baraza la
Mawaziri kabla mahakama hii haijaanzishwa,
zikishapitishwa na Baraza ndipo zitaanza
kutumika,” alisema.
Akifafanua kuhusu mikakati ya udhibiti wa fedha
za miradi ya maendeleo, Waziri Mkuu alisema
kwamba katika bajeti ya mwaka huu, Serikali
imeweza kuongeza kiasi cha fedha zilizotengwa
kwa shughuli za maendeleo kutoka asilimia 27
hadi kufikia asilimia 40.
“Kuongezeka kwa kiwango hiki ni ishara tosha
kuwa tumelenga kutoa huduma kwa Watanzania
na muhimu katika rushwa ni udhibiti wa fedha
hizo na kuhakikisha zinakwenda kwenye miradi;
matuizi mazuri ya fedha za Serikali, matumizi
mazuri ya fedha zinazochangiwa na wahisani ili
ziweze kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” alisema.
“Tumekubaliana na uwepo wa uwazi na
kushirikishana taarifa hasa katika kupeana taarifa
za makampuni yanayoanzishwa na kusajiliwa
katika nchi zinazoendelea kama njia ya kudhibiti
tabia ya nchi ndogo kama Ireland na Panama
kupokea na kuficha fedha zinazotoka kwenye
nchi zinazoendelea” alisema.
Alisema kila nchi imesisitizwa kutumia raia na
kuwalinda watoa siri, kutumia mifumo ya
kiintelijensia, kutumia wanasheria na kuchukua
hatua mbalimbali dhidi ya watu wanaokamatwa
kwa masuala ya rushwa.
Waziri Mkuu alisema alipata fursa ya kukutana
na Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. David
Cameron ambaye mbali na kupongeza juhudi za
Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika
kupambana na rushwa pia aliahidi kutoa mwaliko
ili Tanzania iweze kushiriki kwenye mkutano
mwingine wa masuala ya rushwa utakaofanyika
Japan, Julai mwaka huu.
“Anataka Tanzania iende kwenye mkutano huo ili
ikaelezee mafanikio iliyoyapata katika kukabili
suala hili, ili pia nchi nyingine ziweze kuiga
utaratibu ambao Serikali imeutumia hadi
tukafanikiwa katika mapambano dhidi ya
rushwa,” alisema Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa
amesema ofisi yake haijahusika na kuandaa
mkutano wa wanadiaspora waishio Uingereza
kama ambavyo imedaiwa na baadhi ya watu
kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna watu
maalum wamechaguliwa kushiriki mkutano huo.
Amesema mkutano huo umepangwa kufanyika
kesho (Jumamosi, Mei 14, 2016) na uko wazi
kwa Watanzania wote kushiriki ili waje kusikiliza
nchi yao imefanya nini na kama kuna masuala
yanahitaji ufafanuzi, watapatiwa fursa hiyo.
“Kulikuwa na hofu ya watu wanaotoka mbali
kutoweza kushiriki sababu ya gharama, lakini
nasema yeyote mwenye uwezo wa kuja aje ndiyo
maana tumeuweka muda wa asubuhi ili watu
waweze kushiriki na kuwahi kurudi makwao,”
alisema.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top