Serikal yataja kodi mpya zitakazokatwa.
WAKATI muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka
2016 ukitarajiwa kuanza kujadiliwa bungeni leo
ambao unaoipa serikali mamlaka ya kisheria
kutoza kodi na kutumia fedha hizo, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, ametaja
kodi ambazo zitalazimika kukatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi
kufafanua hoja ambazo hakuzielezea kwa kina
bungeni, Dk Mpango alisema miongoni mwa kodi
hizo ambazo baadhi ya wabunge na vyombo vya
habari vilitetea zisikatwe ni pamoja na Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) katika utalii.
Nyingine ni kutoza kodi katika migahawa na
maduka katika majeshi baada ya kufuta
msamaha wake na kuhamisha jukumu la utozaji
kodi za majengo kutoka halmashauri kwenda
katika Mamlaka ya Mapato (TRA).
Akizungumzia VAT katika utalii, Dk Mpango
alisema kodi hiyo haihusiani na ongezeko au
kupungua kwa watalii nchini kwa kuwa watalii
hao hawatazami kodi hiyo kama kigezo kikuu cha
kwenda kuangalia vivutio vya utalii.
Alitoa mfano wa idadi ya watalii waliotembelea
mbuga za wanyama kwa kipindi 2011 hadi 2014
katika nchi za Tanzania, Kenya na Afrika Kusini,
ambayo inaonesha Tanzania licha ya kwamba
haikuwa ikitoza VAT, bado ilitembelewa na
watalii wachache kuliko nchi hizo ambazo
zilikuwa zikitoza kodi.
Aliendelea kusisitiza kuwa mpaka kabla ya
hotuba yake ya Bajeti ya Serikali ya 2016/17,
nchi zote wanachama wa Jumuiya Afrika
Mashariki zilikuwa zikitoza kodi hiyo kwenye
huduma ya utalii isipokuwa Tanzania ambayo
imependekeza kutoza katika bajeti yake ya
mwaka 2016/17.
Kuhusu uamuzi wa serikali kuhamisha jukumu la
kukusanya kodi za majengo kutoka katika
halmashauri kwenda TRA, Dk Mpango alisema
mamlaka hiyo ya kodi ndiyo yenye uzoefu wa
kutosha katika ukusanyaji kodi za serikali na
ndiyo yenye vituo vya ukusanyaji kodi katika
wilaya na mikoa yote Tanzania.
Kuhusu viwango vya kodi ya majengo, alisema
Waziri wa Fedha na Mipango ataweka viwango
vya kodi ya majengo baada ya kushauriana na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuweka uwazi
na kujumuisha maoni ya wadau wote muhimu
zikiwemo halmashauri husika.
Katika msisitizo mwingine alisema kuwa, mapato
kutokana na kodi ya majengo yataingizwa katika
mfuko mkuu ambao mawaziri wenye dhamana ya
fedha na Tamisemi, ndio watakaoshauriana
kuhusu mgawanyo wa fedha hizo kwa kuzingatia
bajeti za halmashauri husika.
Kuhusu madai kwamba kuondolewa kwa
misamaha ya kodi katika maduka na migahawa
ya vyombo vya ulinzi na usalama kunaondoa
motisha katika taasisi hizo, alisema uamuzi huo
wa serikali upo palepale kwa kuwa misamaha
hiyo ilikuwa ikitumika vibaya.
“Ili kuondoa kasoro hiyo, serikali imeamua
kuweka utaratibu wa kuwalipa posho watumishi
wa vyombo vya ulinzi na usalama ili wanufaike
moja kwa moja kama walengwa. Kiasi cha posho
atakayolipwa askari kitakokotolewa baada ya
mashauriano na vyombo husika,” alisisitiza.
Kuhusu ushuru wa bidhaa kutozwa kwenye ada
ya miamala ya uhawilishaji wa fedha, kama
utaathiri mtumiaji wa mwisho, Dk Mpango
alisema ushuru huo hautakatwa kwenye fedha
zinazotumwa au kupokewa, bali katika ada
inayotozwa na benki au kampuni ya simu.
Alifafanua kuwa kwa sasa sheria inatamka
kwamba ada hiyo itatozwa katika kutuma fedha
tu, hivyo baadhi ya kampuni za simu na benki
zilikuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo
kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati
wa kupokea tu.chanzo habar leo
0 comments :
Post a Comment