Breaking News
Loading...

Advert

Friday, July 29, 2016

CHADEMA yamjibu Msajili wa vya vya siasa Jaji Francis Mtungi.soma zaid.

Baada ya kulifanyia uchambuzi na kulitafakari
tamko la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
lililotolewa jana na msajIli mwenyewe, Jaji
Francis Mutungi tumeona ni jambo lenye afya
kwa ustawi wa demokrasia nchini, kusahihisha
upotoshaji uliomo katika taarifa hiyo ili kuendelea
kumsaidia msajili na watu wengine, watawala na
walio sehemu ya utawala, kuelewa matakwa na
maslahi ya wananchi hasa katika wakati huu
ambao taifa linapitia.
Kwa hakika tumeshangazwa na kauli zilizotolewa
na Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye pia ni
Jaji wa Mahakama Kuu, kutokana na jinsi
ambavyo anaanza kuonesha kuyumba katika
kutimiza wajibu wake hasa kwa kutumia weledi
na ujuzi wake wa sheria kwa kiwango cha nafasi
yake kama jaji.
Katika tamko lake alilolitoa jana na kunukuliwa
na baadhi ya vyombo vya habari jana hiyo na leo,
ameshindwa kuonesha neno hata moja
linaloashiria matusi, kashfa, uongo au hata
kuvuruga amani lililotolewa mbele ya waandishi
wa habari juzi wakati Chama kikisoma hadharani
maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu.
Ni jambo la kushangaza kuwa Msajili Mutungi,
Jaji wa Mahakama Kuu ameweza kuweka vifungu
vingi vya kisheria akidai kuwa vimevunjwa lakini
hawezi kuonesha ushahidi wa namna
vilivyovunjwa au maneno yanayothibitisha
kuvunja hizo sheria. Hii si sahihi hata kidogo na
inakuwa ‘serious’ zaidi inapofanywa na mtu
mwenye weledi wa sheria wa kiwango cha Jaji
Mutungi.
Wakati Jaji Mutungi akinukuu vifungu vya sheria
na kanuni akionekana dhahiri kuwa kuegemea na
kuwatetea watawala ambao wamedhihirisha
kuwa wanatamani nchi irudi enzi za ‘ujima’ wa
fikra za chama kimoja, kwa sababu anazozijua
mwenyewe amesahau au ameshindwa au
amefanya makusudi kwa sababu anazozjijua
mwenyewe, kunukuu kifungu cha 4(1) (e) cha
maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007,
ambacho kinatoa haki kwa vyama vya siasa
kuendesha shughuli zao za kisiasa ikiwemo
mikutano ya hadhara na maandamano kwa
mujibu wa sheria.
Tulidhani kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa ambaye si tu kwamba ni mlezi wa vyama
vyote bali pia anasimama kama mwamuzi wa
mchezo wa mpira uwanjani, katikati ya timu mbili
uwanjani, angelisimamia kifungu hicho muhimu
na kukitumia kuwakemea na kuwaonya watawala,
akiwemo Rais, Waziri Mkuu na Jeshi la Polisi
wasivunje sheria za nchi kuzuia shughuli za siasa
nchini kwa sababu yoyote ile kwa sababu
hawako juu ya sheria za nchi hii.
Aidha, sasa tunaanza kushtuka na kuanza
kujiuliza maswali mengi kuhusu kasi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa kujijengea utaratibu
usiokuwa na kawaida kwa nafasi yake ya kisiasa
na kisheria, kuwa na kasi ya ajabu kutoa kauli au
matamko yanayoonesha kuwatetea/kuwalinda
watawala wanapovunja sheria zinazosimamia
vyama vya siasa. Jaji Mutungi amekuwa mahiri
wa kuvikemea au hata kuvionya vyama vingine
tofauti na CCM, kila vinapodai haki za kisiasa
ambazo ziko na zinapaswa kutekelezwa kwa
mujibu wa sheria, wala si kwa hisani ya mtu
yeyote.
Waandishi wa habari na umma kwa ujumla
watakuwa mashahidi kwa namna ambavyo CCM
wamekuwa wakitumia vyombo vya dola,
kuvikandamiza, kuvinyanyasa, kuviwekea
mazingira magumu na kuvinyima haki za kufanya
siasa vyama vingine washindani wake kwa ajili tu
ya kulinda maslahi ya chama kilichoko
madarakani.
Katika hali hiyo ambayo hata imekuwa
ikisababisha mauaji na umwagaji damu za watu
wasiokuwa na hatia kwa sababu tu ni wafuasi wa
vyama vingine, Msajili wa Vyama vya Siasa
hajawahi kuthubutu kujitokeza hadharani
kuwaonya na kuwakemea CCM na walioko
serikalini kuwa kutumia vyombo vya dola kwa
manufaa yao ya kisiasa ni kosa kwa mujibu wa
sheria za nchi kupitia kifungu cha maadili ya
vyama vya siasa cha 5(1)(c), za mwaka 2007.
Tulitegemea kwa kutumia umahiri huo huo wa
kunukuu vifungu vya sheria na kanuni za maadili
ya vyama vya siasa ambao Msajili amekuwa
akiuonesha dhidi ya vyama washindani wa CCM
kila vinapodai haki za msingi za kisiasa,
angekuwa ameutumia pia kuwakemea, kuwaonya
au hata basi kuwakumbusha CCM na Rais
Magufuli kwa kutumia kifungu cha 5(1) (i) cha
kanuni za maadili ya vyama vya siasa za Mwaka
2007, kuwa ni makosa kutumia mamlaka,
rasilimali za serikali, vyombo vya dola au wadhifa
wa kiserikali, kuvikandamiza vyama vingine kwa
manufaa ya kisiasa ya upande mmoja.
Si hayo tu, Jaji Mutungi ama aliamua kuwa kimya
au alikuwa na kigugumizi aliposikia;
1. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais John
Magufuli na Jeshi la Polisi wakitoa kauli
kinyume cha sheria wakitangaza na kuagiza
kuzuia shughuli za kisiasa nchini kwa
matakwa yao tu.
2. Mabalozi na wanadiplomasia wakizuiwa
kukutana na asasi zisizo za kiserikali au
vyama vya siasa.

Kukiukwa kwa misingi ya sheria, kanuni na
taratibu za nchi katika uteuzi wa wakurugenzi
na makatibu tawala.
1. Hali tete inayoendelea Zanzibar baada ya
watawala kuharibu uchaguzi mkuu mwaka
jana kisha wakafanya uchaguzi wa marudio
kwa maslahi ya CCM, kinyume kabisa na
sheria za nchi.
Hayo ni baadhi tu ya masuala ya muhimu
ambayo ofisi ya msajili ilitarajiwa kuwa ingekuwa
mstari wa mbele kukemea na kuonya ili kuweka
mizania ya ushindani wa kisiasa katika usahihi
wake.
Kwa mwenendo huu ambao usipoangaliwa na
kufanyiwa kazi ya kuurekebisha haraka,
tunachelea kusema kuwa Ofisi ya Msajili na Jaji
Mutungi mwenyewe wataanza kujikosesha uhalali
machoni pa Watanzania ambao wasingependa
kuona siasa ambayo ni maisha yao, ikifananishwa
kama vile ni jambo la kawaida tu lisilokuwa na
maana.
Kupitia taarifa hii, tunamtaka Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Mutungi kuwa makini na utaratibu
huo vinginevyo Watanzania wataanza kuiweka
ofisi yake na yeye mwenyewe kwenye kapu moja
na aliyekuwa mtangulizi wake, ambaye ilifika
mahali wananchi walimuona yeye binafsi, kupitia
kauli zake, matendo yake na ofisi yake kwa
ujumla, sawa na sehemu ya chama kilichoko
madarakani.
CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani
nchini hakiwezi kuvumilia wala kukubali hiki
kinachoanza kujionesha kuwa ni ‘ double
standards’ za mtu anayetarajiwa kuwa mlezi na
refarii, kujitokeza hadharani pale tu ambapo
maslahi ya chama tawala na watawala
yanapoguswa lakini anakuwa kimya na hata
kuweka masikio nta mara vyama washindani wa
CCM vinapokandamizwa, kinyume kabisa cha
sheria.
Kama chama chenye wanachama na viongozi
wanaojua haki na wajibu wao wa kikatiba na
kisheria, tutaendelea kufanya shughuli za kisiasa
kwa namna itakayosimamia haki na matumaini
ya wananchi kwa ajili ya amani na utulivu wa
kweli, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
za nchi si kwa kufuata matamko, kauli au
maelekezo ya mtu yeyote.
Ni kwa kuzingatia dhana hiyo, maana Kamati Kuu
katika kikao cha dharura kilichofanyika mwishoni
mwa juma lililopita na maazimio yake
kutangazwa juzi Jumatano, moja ya maazimio
yake ni kuanzisha operesheni ya UKUTA (Umoja
wa Kupinga Udikteta Tanzania) ambayo inalenga
kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali
tofauti zao zozote zile, kudai haki na matumaini
dhidi ya udkiteta katika nchi yao na kuzuia
harakati za watawala kuataka kupora mamlaka
ya wananchi na kujiweka juu ya sheria kwa
namna ile ile ambayo madikteta hufanya.
Imetolewa leo Ijumaa Julai 29, 2016 na;
Prof. Mwesiga Baregu
Mjumbe wa Kamati Kamati Kuu

0 comments :

Post a Comment

Back To Top