Breaking News
Loading...

Advert

Friday, July 29, 2016

Mpango wa UKUTA walaniwa na Taasisi na wadau mbalimbali hapa nchini.soma zaid.

SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kutangaza nia ya
kufanya mikutano ya hadharani nchini kote
kuanzia Septemba Mosi kutokana na sababu
mbalimbali, taasisi na wadau mbalimbali
wamelaani mpango huo.
Akizungumzia hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, Jaji Francis Mutungi amesema
amepokea kwa masikitiko makubwa tamko hilo,
huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijitokeza
na kulaani mpango huo.
Wengine waliopinga mpango huo ni wasomi
wakiwemo Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam anayejipambanua katika siasa za
upinzani, aliyewahi kuwa mwanachama wa
Chadema, Dk Kitila Mkumbo na wachambuzi wa
Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk
Benson Bana na Dk Bashiru Ally.
Msajili vyama vya siasa alaani
Akizungumzia tamko hilo la Chadema, Jaji
Mutungi alisema limejaa lugha ya uchochezi,
kashfa, kuudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu
wa amani.
Alisema kimsingi Sheria ya Vyama vya Siasa
namba 5 ya mwaka 1992 kifungu (2) (c)
inakataza chama cha siasa kutumia au
kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu
kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.
Alisema aidha kifungu cha 9 (2) (f) kinakataza
chama cha siasa kuruhusu wanachama au
viongozi wake kutumia lugha ya matusi, kashfa
na uchochezi ambayo inaweza kusababisha au
kupelekea kutokea uvunjifu wa amani.
Alisema pia kanuni ya Maadili ya Vyama vya
Siasa, Tangazo la Serikali namba 215,
linakataza chama cha siasa kutumia lugha za
matusi, kashfa, uongo na uchochezi.
Alisema Kanuni ya 5 (1) (d) inakitaka chama
cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi
ambayo ni uongo, kuhusu mtu yeyote au chama
cha siasa chochote. “Hivyo tamko la Chadema
ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Aidha, hii si mara ya kwanza kwa Chadema
kutumia lugha za namna hii za kuhamasisha
uvunjifu wa amani.
“Natumia fursa hii kukemea tamko hilo
hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6 (2) ya
Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, pia
nawaasa Chadema wasiendeleze tabia hii,”
alisema Jaji Mutungi.
Alisema dhamana aliyopewa kama Msimamizi
wa Sheria ya Vyama vya Siasa kazi yake ni
kuviasa vyama vyote vya siasa vitimize wajibu
wao kwa weledi kama taasisi za kisiasa.
“Ni vyema viongozi wa vyama vya siasa
wakaonesha taswira stahiki ya wanasiasa
wakomavu, au vyama vya siasa vya kutolea
mfano ndani na nje ya mipaka yetu, kwa
kuzingatia sheria za nchi katika kuendesha
shughuli za kisiasa. “Vyama vya siasa viepuke
vitendo, kauli au matamshi yenye mlengo wa
kusababisha uchochezi au kufarakanisha umma
na serikali yao. Navisihi kuzingatia utaratibu wa
mawasiliano kwa mujibu wa sheria zilizopo,
aidha uvumilivu wa kisiasa katika azma za
kudumisha ukuaji wa kidemokrasia nchini
haukwepeki,” alisema Jaji Mutungi.
CCM wajibu mapigo
Katika hatua nyingine CCM imeionya Chadema
kuacha kupotosha umma na kutaka
kuwaaminisha wananchi uongo wanaoutunga ili
kujaribu kupata wafuasi.
Aidha, imewataka Watanzania kupuuza
maandamano yaliyopangwa kufanywa na
Chadema kwa kuwa ni ishara ya kuchochea
uvunjifu wa amani, huku ikiwataka viongozi hao
wanaoshinikiza maandamano kuandamana na
familia zao.
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka
alisema Dar es Salaam jana kuwa tamko
lililotolewa na Chadema la kupanga kufanya
mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia
Septemba Mosi mwaka huu, limejaa uongo na
ubabaishaji na linaonesha kuwa wapinzani
wamekosa ajenda na njia pekee wanayoona
inafaa ni kutunga utapeli, uongo na uzushi.
Alisema kimsingi hoja walizotumia kufikia
uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa upotoshaji na
uongo uliokithiri.
Alisema kwa mfano chama hicho kimekuwa
kikidai serikali imezuia mikutano yote ya vyama
vya siasa huku wakijua jambo hilo si kweli. “…
Wamekuwa wakisema hivyo huku wakijua kuwa
ni uongo kwani serikali haijazuia mikutano.
Kwenye majimbo wabunge wao wako huru
kufanya shughuli zao, tumeona wabunge
wakifanya mikutano kwenye majimbo ikiwemo
wa upinzani,” alisema Ole Sendeka.
Alisema vyama vya siasa kufanya shughuli zao
kwa mujibu wa Katiba si kosa na wala si jambo
ambalo limezuiliwa na ndio maana
imeshuhudiwa vyama vya siasa vikifanya
mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Ole Sendeka alisema jambo lingine ambalo ni
hoja za uongo na uzushi ni kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano ni ya kidikteta, na alihoji
udikteta wanaousema Chadema ni upi? “Ni huu
wa kushughulikia watumishi hewa, ni huu wa
kuwabana wakwepa kodi, ni huu wa kupunguza
na kudhibiti safari za nje, ni huu wa kubana
matumizi ya serikali, ni huu wa kufukuza
wazembe na wabadhirifu kazini? “Hivi udikteta
huo ni huu wa kushughulikia mafisadi na mpaka
kuanzisha Mahakama yao?” Alihoji Msemaji
huyo wa CCM.
Alisema CCM inaamini Watanzania wengi
wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na
Rais John Magufuli na serikali yake, lakini kama
hatua hizo Chadema inaona ni udikteta bila
shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu na ndio
maana wako tayari kuleta vurugu.
Wasomi UDSM wafunguka
Wakitoa maoni wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Profesa Mkumbo, Dk Bashiru na
Bana walikosoa mpango huo wa Chadema.
Profesa Mkumbo alisema vyama vya siasa vina
wajibu wa kulinda misingi ya demokrasia lakini
pia vina haki ya kupigania kufanya shughuli za
siasa ingawa si kwa mapambano.
Alisema ni muhimu vyama vya siasa kujenga
amani ya nchi lakini akasema ni muhimu pia
kwa Jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu
kupinga mikutano ya hadhara kwa vyama vya
siasa.
“Pande zote mbili yaani Jeshi la Polisi na vyama
vya siasa vipeane nafasi kila mmoja, bila
kuvuruga shughuli za maendeleo, kulindwa kwa
demokrasia na kuiendeleza,” alisema Profesa
Mkumbo.
Naye Dk Bashiru alisema kauli ya kufanya
mikutano nchi nzima ni vyema ikafafanuliwa,
kuhojiwa au kutafsiriwa na taasisi za
kidemokrasia ikiwemo Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ambayo inasiamamia sheria
za vyama vya siasa.
Alisema taasisi hiyo itoe ufafanuzi kwa
kuzingatia sheria ili kuongoza kauli na vitendo
vitolewavyo na vyama vya siasa katika kukuza
demokrasia, pamoja na kuangalia matakwa ya
wanasiasa ili isiwe ni kuvuruga misingi ya
mamlaka.
Alisema hakuna mahali utaratibu, sheria na
kanuni zinafuatwa kiholela, na kwamba uholela
haujengi demokrasia bali ni chanzo cha chuki na
hata kuumiza, hivyo yawepo mazungumzo ili
kufikia muafaka na kama yupo asiyeridhika
aende Mahakamani.
Kwa upande wake Dk Bana alisema kukaidi
agizo linalotolewa na vyombo vya dola sio
jambo jema na kwamba ni vyema kuheshimu
ikiwa ndio njia ya kukuza demokrasia. Alisema
kama chama hicho kinaona hakiridhiki na
maagizo hayo wanaweza kutafuta ufumbuzi
wake kwa kwenda Mahakamani ili kuitafuta
huko.
Akizungumzia sakata hilo, Dk Bana alisema
mpango huo si suluhisho la maridhiano ya
kisiasa na badala yake utaleta vurugu na
kuchochea uvunjifu wa amani.
Alisema Chadema wanapaswa kuachana na
mpango huo na badala yake waombe kuonana
na Rais Magufuli na viongozi wengine wa
Serikali ili kuwasilisha hoja zao kuhusu mambo
wanayoona hayaendi sawa, akisema Rais
Magufuli ni msikivu.
‘Kutumia ubabe hakuwezi kuzaa mwisho
mwema kwao, wangeweza pia kulitumia Bunge
lakini walilikwepa, hivyo si njia za kiungwana
kufanya mikutano hiyo kwa nchi nzima na
watambue kuwa hawatoungwa mkono,” alisema
Dk Bana.
Kuhusu kumwita kiongozi wa nchi dikteta, Dk
Bana alihoji kama kitendo cha kutumbuliwa kwa
majipu na mafisadi kimewaudhi au walitaka
atumie sindano kubwa ama ndogo ili aweze
kutimiza azma hiyo na wao waweze kufurahia.
Alisema Watanzania wameshaona mwanga
wakitambua kuwa Rais Magufuli ndiye kiongozi
wamtakaye na anaongoza serikali waitakayo na
hivyo ni vigumu kuwaaminisha vinginevyo kama
wanavyotaka kufanya Chadema.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top