Wazir mkuu amesema uamuzi wa kufuta tozo tano kati ya tisa wa korosho uko pale pale.soma zaid.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo tano kati ya
tisa alizokuwa anakatwa mkulima wa zao la
korosho uko pale pale na unatarajiwa kuanza
kutumika katika msimu mwaka huu hivyo
ameitaka Bodi ya Korosho kusimamia uamuzi
huo.
“Watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali
mnatakiwa kuhakikisha kwamba maelekezo haya
yanafuatwa. Malengo yetu ni kumpunguzia
mkulima mzigo wa tozo nyingi alizokuwa
anakatwa,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumamosi, Julai 16, 2016) wakati akipokea
taarifa ya maendeleo ya mkoa Mtwara pamoja
na taarifa ya kuondolewa kwa baadhi ya tozo
katika zao la korosho zilizowasilishwa na Mkuu
wa Mkoa huo, Halima Dendego.
Alisema Serikali iliamua kuzifuta tozo hizo
baada ya kubainika kuwa zilikuwa zikiwanyonya
wakulima hali iliyosababisha wauchukie mfumo
wa stakabadhi ghalani.
“Kuanzia mwaka huu Serikali imeamua
mfanyabiashara yeyote wa korosho hana budi
kuanza kulipa malipo ya awali kabla ya kuingia
kwenye mnada ili tuwe na uhakika wa kununua
korosho hizo na kuwalipa wakulima kwa wakati,”
alisema.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya kushuka
kwa uzalishaji wa korosho Waziri Mkuu aliutaka
mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao hilo ufanye
utafiti wa kubaini sababu ili waweze kutafuta
namna ya kuipatia ufumbuzi.
“Nitakuja kukutana na viongozi wa mfuko
waniambie wanafanya nini na wamefanya nini
miaka mitatu iliyopita na wana mpango gani huko
mbele tunakokwenda kama hakuna mpango
tutauangalia mara mbili mbili kwani wana fedha
nyingi lakini hata mbegu hawapeleki kwa
wakulima,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliitaka Bodi
ya Korosho kuhakikisha kila msimu wakulima
wanapata pembejeo bora na zinawafikia kwa
wakati ili waweze kupata mazao ya kutosha.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 17, 2016
0 comments :
Post a Comment