Baraza la Tiba Asili kortini kwa kufuta lesseni za kutoa huduma za kitabibu(Tiba Asili).soma zaid
MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na Mbadala
akiwemo mmiliki wa Kliniki ya Sure Herbal,
Simon Rusigwa wamewasilisha maombi ya
kuomba ruhusa ya kufungua kesi ya kupinga
uamuzi wa kufutiwa leseni za kutoa huduma za
kitabibu.
Wamewasilisha maombi hayo katika Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, dhidi
ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG).
Mbali na Rusigwa, matabibu wengine
waliowasilisha maombi hayo kupitia kwa Wakili
Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah Mandai wa
kliniki ya Mandai Herbalist, Fadhili Kabujanja wa
Fadhaget Sanitarium na John Lupimo wa
Lupimo Sanitarium.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa jana mbele
ya Jaji Ama–Isario Munisi wa mahakama hiyo,
hata hivyo kabla ya kuanza kusikilizwa, Serikali
iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa
maombi hayo hayakufuata misingi ya kisheria.
Katika pingamizi hilo serikali inadai kuwa
maombi hayo yana kasoro kwa kuwa waombaji
hawajapita njia zote zinazotakiwa wazifuate
ndipo waende mahakamani pia wanadai maombi
hayana miguu ya kusimamia kwa kuwa hati ya
viapo vya walalamikaji vina upungufu ya
kisheria.
Baada ya kuwasilishwa kwa pingamizi, Jaji
Munisi aliahirisha shauri hilo hadi kesho saa 8
mchana, ambapo alizitaka pande zote
zinazohusika ziwepo ili kusikiliza pingamizi hilo.
Katika maombi yao, matatibu hao wanadai,
wameamua kupeleka maombi hayo mahakamani,
kwa kuwa wanaamini walifutiwa leseni bila
kufuata taratibu za kisheria.
Wamedai wanaamini uamuzi uliochukuliwa
umetolewa bila kupitia Kamati ya Maadili ya
Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, huku wakidai
kuwa huo si uamuzi bali zilikuwa tuhuma mpya,
lakini hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.
0 comments :
Post a Comment