Lowassa afunguka na kuongea maneno haya.soma zaid.
Asema hana kinyongo naye, amvaa JPM
*Agusia mikakati ya kuingia Ikulu 2020
Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia
Ukawa, Edward Lowassa, amemtaka Rais
mstaafu Jakaya Kikwete, ajihukumu mwenyewe
kutokana na matendo aliyoyafanya dhidi yake.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika
mahojiano yaliyorushwa na kituo cha Luninga
cha Azam kupitia kipindi cha Funguka
kilichoongozwa na mtangazaji mkongwe, Tido
Mhando, huku akisema hana kinyongo na
Kikwete.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipoulizwa kuhusu
uhusiano wake na rais huyo mstaafu wa awamu
ya nne, ambapo wawili hao walikuwa maswahiba
wakubwa, lakini walikuja kutofautiana wakati wa
mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia
CCM mwaka jana.
“Siwezi kumhukumu Kikwete (Jakaya) yeye
mwenyewe ila wengine wamuhukumu na yeye
ajihukumu mwenyewe, sijamwona hivi karibuni
lakini sina kinyongo naye,” alisema Lowassa
ambaye kwa sasa ametimiza mwaka mmoja
tangu alipojiunga na Chadema Agosti mwaka
jana.
Kutokana na hatua hiyo Lowassa pamoja na
watu waliokuwa wakimuunga mkono ndani ya
CCM waliweza kufunguliwa mafaili ndani ya CCM
sambamba na kufuatiliwa nyendo zao, ambapo
wakati wa mchakato huo jina la mwanasiasa
huyo lilikatwa na Kamati ya Maadili chini ya Rais
mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye alikua
mwenyekiti wa CCM taifa.
AMANI NA HATI MILIKI
Pamoja na mambo mengine, Lowassa ambaye
pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,
alisema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu amani
ya nchi na kwamba hakuna mwenye hati miliki.
Kutokana na hilo, alimtaka Rais Dk. John
Magufuli, kuwa na utamaduni wa kufanya
mazungumzo na wanasiasa ili kufikia mwafaka
wa mambo ya kisiasa nchini.
“Serikali inatakiwa kuwa na tabia ya kuzungumza
na si kutumia ghadhabu, sisi wote ni Watanzania
kwanini tunaogopa kuzungumza. Siku zote
mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia
maridhiano,”alisema.
ZUIO LA MIKUTANO
Akizungumzia kuhusu mikutano ya siasa kuzuiwa,
Lowassa alieleza kushangazwa kwa kitendo cha
Rais Magufuli kupiga marufuku hiyo huku yeye
akizunguka kufanya mikutano ya hadhara.
Alisema kwa kuwa aligombea urais mwaka jana
na akachaguliwa na Watanzania milioni sita hivyo
ana haki ya kuzunguka mikoani kuwashukuru
waliompigia kura.
Pia alishangazwa na barua ya Msajili wa Vyama
Siasa, akisema imejaa ghadhabu na si uongozi.
“Yeye anakwenda Kahama (Rais Magufuli)…
kuwashukuru wananchi anafanya mikutano ya
hadhara kwa nini na mimi nisiende Mbeya na
Iringa kushukuru. Nimeona barua ya msajili
imejaa ghadhabu zaidi si uongozi,”alisema
Lowassa.
OPERESHENI UKUTA
Akizungumzia kuhusu operesheni Ukuta
iliyozinduliwa hivi karibuni na Chadema, Lowassa
alisema ni sahihi huku akisisitiza yafanyike
mazungumzo kabla ya kufikia Septemba Mosi,
mwaka huu.
“Yafanyike mazungumzo ya kushughulika na
mambo haya kabla ya kufika Septemba Mosi,
haiwezekani chama cha siasa eti hakuna siasa
mpaka mwaka 2020…hili lazima litazamwe.
“Ukitoa amri, amri, amri za kiimla tuzungumze
kila mtu anaheshimu amani ya nchi hii,
tuzungumze tutaelewana,”alisema.
Alisema mtu akitaka kuvuruga maendeleo huanza
kuvuruga vyama vya siasa.
NINGEFANYA VIZURI ZAIDI YA JPM
Alipoulizwa tathmini yake kuhusu utawala wa
Rais Dk. Magufuli, alisema anafanya vizuri lakini
ingekuwa yeye asingeanza na madawati bali
angeanza na masilahi ya walimu.
“Magufuli anafanya vizuri katika maeneo fulani
lakini mimi ningefanya vizuri zaidi, kama
nilivyosema kipaumbele changu ni elimu, elimu,
elimu…nisingeanza na madawati, ningeanza na
masilahi ya walimu.
“Madawati ni sehemu ndogo sana ya elimu,
wangechukua kwa ujumla na si madawati tu. Sisi
upinzani tungeanza kwa ujumla wake, Serikali
inapaswa ishughulike na mambo makubwa,
madawati ni kazi ya makatibu kata.
“Kuna maeneo kwa maoni yangu ni muhimu zaidi
ajira, lipo tatizo la ajira hapa nchini. Ajira
haitazamwi mama ntilie, bodaboda
tunawakimbiza barabarani hawana ajira.
“Kuna jambo lingine asaidiwe Rais, Serikali
inatakiwa iheshimu mihimili mitatu, mfano
alikwenda mahakamani siku ya Law Day (Siku ya
Sheria), akawaambia mkimaliza kesi zangu
haraka na mkawatia hatiani nitawapeni hela ya
kujenga majengo yenu, nadhani hakuwa na
maana hiyo lakini ilitafsiriwa kwamba anatoa
hongo,”alisema Lowassa.
AJIVUNIA SHULE ZA KATA
Lowassa alisema anamshukuru Mungu kushika
bendera ya kusimamia shule za kata wakati
akiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya nne.
“Namshukuru Mungu kushika bendera ile,
najivunia kwa kweli nafurahi shule moja
iliyoongoza ni ya kata. Naamini leo (jana), zile
shule zingekuwa mikononi mwangu zingekuwa
mbali zaidi na bora,” alisema.
WABUNGE UKAWA
Akizungumzia mwenendo wa Bunge, Lowassa
alisema tatizo kubwa kwa ujumla wake ni
kutokana na Spika wa Bunge, Job Ndugai,
kutokuwapo bungeni.
Alisema tatizo lingine ni la kisaikolojia kutokana
na Naibu Spika, Dk.Tulia Ackson, kuwapo katika
nafasi hiyo kwa njia ambayo wengine wanaona si
sahihi.
“Tatizo katika ujumla wake ni kutokana na
Ndugai kuwa na hali mbaya ya afya namfahamu
ni mtu makini sana…angekuwapo yale mambo
yasingefikiwa.
“Kuna tatizo la kisaikolojia Naibu Spika amekuwa
katika nafasi ile kwa njia ambazo pengine
wengine wanaona si sahihi anachukua maamuzi
ambayo ni magumu kidogo naelewa wabunge
wetu kuchukua hatua ile ni sahihi…wangefanya
nini?
“Siku ambayo wamejiweka plasta midomoni,
Marekani nao walikuwa wamekaa chini mpaka
asubuhi kupinga hoja ya Serikali, hivyo ni njia ya
ku-express (kufikisha), kutoridhika kwao,
walistahili kufanya hivyo kwa sababu haki yao
haikusikilizwa.
“Wangekubali kuzungumza…bajeti imepita bila
upinzani, hii si salama kwa demokrasia …siasa ni
kuzungumza, naona ndicho kinachokosekana,”
alisema Lowassa.
KUHAMIA DODOMA
Alisema viongozi wa awamu zote walikuwa na
dhamira ya kuhamia Dodoma lakini kutokana na
matukio fulani fulani makubwa mambo
yanabadilika.
“Ninawatakia heri lakini wasiende kwa kasi sana
wasije wakavunjika miguu.. utekelezaji wa
kuhamia Dodoma ufanyike kisayansi, wanaweza
kuchukua fedha za miradi ya maendeleo ili
kuhamia Dodoma,”alisema.
MWAFAKA Z’BAR
Kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, Lowassa
alimwomba Rais Dk. Magufuli, kulitazama suala
hilo kwa kuwa hawezi kulikwepa na kwamba
mwaka 2020 ni mbali kusubiri mwafaka.
“Namwomba Rais alitamaze hili la Zanzibar ni
sehemu ya nchi yetu, mambo yanayotokea kama
ni kweli yanatia kichefuchefu, kuna sauti ya watu
wengi tusipuuze.
“Rais alisema si suala lake lakini hawezi
kukwepa, watu wanakamatwa wanafungwa,
Amani Karume alifanya vizuri kuleta Serikali ya
maridhiano,” alisema.
Mwanasiasa huyo alisema kinachotakiwa kwa
sasa ni kufanyika mazungumzo kwa sababu watu
wakionewa kwa muda mrefu wanachukua
maamuzi ya hamaki.
“Kwanini usizungumze nao badala yake
unachukua uamuzi tu. Aliniambia Maalim Seif
tupewe kibali uchaguzi usimamiwe na AU (Umoja
wa Afrika) tusiachie watu wanaumia,
tuzungumze na tukisema tusubiri mwaka 2020
miaka hiyo ni mingi sana lazima tuzungumze
tukafikiri amani ni salama.
“Wakati ule hata mimi walitaka nitangaze
matokeo na pengine hali ingekuwa tofauti kidogo,
watu hawakuridhika…kwanini tusizungumze,
kuchukua ubabe tu hapana bwana please ni
maisha ya watu. Tumekatiwa misaada na MCC
na miradi imesimamishwa,”alisema Lowassa.
KATIBA MPYA
Akizungumzia kuhusu Katiba Mpya, alisema hilo
ni suala gumu na kwamba linahitaji fikra mpya,
kuvumiliana.
“Serikali haijatoa muda wa mazungumzo
ilichukuliwa ghadhabu mpaka leo hatuna Katiba,
tuzungumze…Katiba ni suala gumu linahitaji
muda mrefu wa kuelewana. Fikra mpya,
kuvumiliana na research (utafiti) ,”alisema
Lowassa.
UTEUZI
“Zamani ili upate ajira kama hizi ulikuwa vetted
(utathiminiwe). Siku hizi inakuja kugundulika
mteuliwa si raia siku anaapishwa. Tusiwe
intimidated (tunatishwa) na elimu, kwamba huyu
kasoma sana.
“Kuna watu wana PhD (Shahada ya Uzamivu),
lakini wanafanya kazi vizuri. Katika mkutano
mmoja Mwalimu Nyerere (Julius) alipata kusema
kwamba Profesa anashikilia kitu kimoja kidogo
mambo mengi hayajui…sasa hii ya amesoma,
amesoma si kigezo pekee kuna uadilifu na
uzalendo,”alisema Lowassa
URAIS 2020
“Wataniona Ikulu 2020, sina mashaka tukiwa na
Katiba nzuri njia ni nyeupe… si vizuri kueleza
mikakati yangu. Ukifanyika uchaguzi wa haki na
kweli huku tume ikiwa huru, sina
wasiwasi,”alisema.
UCHAGUZI 2015
“Haukuwa sawa hata kidogo… tuache mambo
haya uchaguzi umeshamalizika tutaumizana
mioyo bure, nina imani na upinzani tuna nguvu
sana,” Lowassa alisema hayo alipotakiwa
kuzungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
0 comments :
Post a Comment