MCT yampongeza Rais magufuli kupambana na rushwa.soma zaid
BARAZA la Habari Tanzania (MCT)
limeipongeza serikali ya Rais John Magufuli kwa
jitihada zake za kupambana na rushwa pamoja
na ubadhirifu na kusema inapaswa kuungwa
mkono na kila mmoja na pia vyombo vya habari.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga
alitoa pongezi hizo jana wakati wa Mkutano
Mkuu wa 18 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar
es Salaam.
Mukajanga alisema kwa kuwa vyombo vya
habari ni namba moja katika kupambana na
rushwa, wanaiomba serikali itafute suluhu pale
vinapokosea badala ya kuvifungia.
“Midhali serikali inajua sheria zilizopo zinahitaji
marekebisho, tupunguze kuzitumia kwa sababu
hazitupeleki mbele, bali zinaturudisha nyuma,”
alisema Mukajanga.
Alisema hivi sasa Kamati ya Maadili ya Baraza
hilo ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Juxon Mlay
inaendelea kukusanya ushahidi wa kutosha ili
waende kuzungumza na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
kuhusu mgogoro huo wa kuvifungia vyombo vya
habari.
Vyombo vya habari vilivyofungiwa na serikali
hivi karibuni ni gazeti la Mseto na vituo vya
redio vya Magic FM na Radio Five. Naye Rais
wa baraza hilo, Jaji Thomas Mihayo alivitaka
vyombo vya habari pamoja na waandishi wa
habari visiogope kutumia haki yao ya msingi
pale inapotokea wanavunjiwa uhuru wao wa
kujieleza kwa sababu mahakama ni sehemu
sahihi ya kudai haki kamili.
“Watanzania wengi hawapendi kutumia vyanzo
sahihi vya kuweza kupata haki yao. Waandishi
wa habari mnapotaka kupata haki yenu nendeni
mahakamani kwa sababu ni chombo cha pekee
kinachoweza kutoa haki ya kweli," alisema Jaji
Mihayo.
Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye
ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti la
MwanaHalisi, Said Kubenea alisema kuna tatizo
kwa waandishi wa habari kuwa wavivu katika
kutafuta haki mahakamani, pengine ni kutokana
na mchakato mrefu.
Aliiomba MCT kuwa mstari wa mbele katika
kuzisimamia kesi hizo mahakamani, kwa kuwa
kwa kufanya hivyo kutaipa kesi hizo nguvu.
“Ni rai yangu MCT, lisimame katika kutetea
waandishi na vyombo vya habari," alisema
Kubenea. Katika hilo, Mukajanga alisema hilo ni
jukumu lao wamelipokea hivyo watatenga fedha
kwa ajili ya kusaidia uhuru wa habari nchini.
0 comments :
Post a Comment