Mkakati wa mbowe katika kufanikisha mikutano na maandamano septemba mosi.soma zaid
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana
alitangaza mkakati wa chama hicho kufanikisha
mikutano na maandamano ya walichokiita
Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta),
huku jeshi la polisi nao wakijiandaa kukabiliana
nao.
Mbowe aliitaja mikakati hiyo ikiwamo kamati za
kuhamasisha Ukuta ambapo aliyekuwa
mgombea urais kupitia Ukawa Edward Lowassa
amepangiwa Mbeya, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Vincent Mashinji atakuwa Mwanza, Makamu
Mwenyekiti Profesa Abdallah Safari atakuwa
Tabora huku Mwenyekiti wa Bawacha Taifa,
Halima Mdee na Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema Mabere Marando wakipangiwa Dar es
Salaam.
Alisema yeye (Mbowe) ataongoza Kanda ya
Kaskazini wakati Profesa Mwesiga Baregu
amepewa jukumu la kufafanua Ukuta kwa
taasisi za kimataifa, viongozi wa dini na
wastaafu.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu
Lissu na mawakili 12 wao watajifungia Dar es
Salaam kufungua kesi 21 kutetea mikutano.
Lakini, Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa
rasmi baadaye huku CCM wakisisitiza msimamo
wao wa kupinga maandamano hayo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera
Bulimba alisema jeshi hilo litatoa taarifa siku
chache zijazo. “Tutawaita na tutazungumza,
naomba tujaribu tu kuvuta subira,”alijibu kwa
ufupi msemaji huyo wa polisi.
Hata hivyo kikosi cha Askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) katika mikoa mbalimbali
ikiwamo Dar es Salaam na Kilimanjaro
walionekana wakifanya mazoezi wakiwa na
silaha na magari ya maji ya kuwasha kwa siku
tofauti.
CCM watoa ushauri
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka
alisema licha ya chama kuzungumza mara
kadhaa, wanatarajia kutoa tamko kwa lengo la
kuwaeleza Watanzania tahadhari juu ya mchezo
unaojaribiwa na Chadema.
Sendeka alisema viongozi wa dini na makundi
mbalimbali yameshauri juu ya mipango yao,
lakini hawataki kusikia.
“Jambo hilo limezungumzwa mara nyingi sana,
viongozi wa dini wameshasema, watu wenye
mapenzi na nchi yao wakishauri waache huo
mchezo wao ambao sidhani kama watafanikiwa,
kwa hivyo tunatarajia kutoa tamko letu siku
yoyote kuanzia kesho (leo),”alisema.
Mbowe na safu yake
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa
viongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini jana
katika Hoteli ya Coridol Springs jijini hapa,
Mbowe alisema chama hicho kimejipanga
kufanya mikutano na maandamano ya amani
nchi nzima Septemba Mosi ili kutetea utawala
wa sheria na Katiba.
Mbowe alisema Rais Magufuli aliapa kuilinda
Katiba, Wabunge waliapa kuilinda Katiba,
madiwani waliapa kuilinda Katiba ili nchi
iongozwe katika misingi ya sheria na utawala
bora.
Alisema haiwezekani nchi kuongozwa kwa
matamko ambayo yanakiuka katiba na Chadema
kama chama kikuu cha upinzani kina wajibu wa
kuishauri na kuikosoa serikali na hawawezi
kukaa kimya.
Alisema matamko ya Rais kuwa hakuna ruhusa
ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama
vingine na kuacha chama chake kufanya
mikutano na pia kuzuia mikutano hadi mwaka
2020 haikubaliki.
“Sisi tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria
na siyo matakwa ya viongozi ambayo yanakinzana
na sheria na Katiba ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema wanafanya mikutano na maandamano
kama sehemu ya kueleza malalamiko yao, hasa
kutokana na kauli za viongozi ambazo zinakiuka
sheria.
Mbowe alisema vyama vyote vikiamua kukaa
kimya na kuacha mambo yaliyotokea Zanzibar,
yaliyotokea Dodoma na yanayotokea sasa
kutokana na kauli za viongozi, ni wazi nchi
haitakuwa salama.
“Tukiamua sote kujifanya wanafiki kusema hewala
nchi haitakuwa salama itazaa taifa la watu wenye
hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu
kuanzia sasa kufanya kazi kila siku kuisaidia
sekretarieti,” alisema.
Mbowe alisema kutokana na unyeti wa Ukuta,
Kamati Kuu ya Chadema imeunda kamati ndogo
tano, ambazo zitasaidia kufikiwa malengo
yaliyokusudiwa kwa kuhusisha taasisi na
vyombo vingine.
Alisema pia kuna kamati ya maandalizi ya Ukuta
ambayo tayari imeanza kazi ya kufafanua
maamuzi ya kamati kuu, ambayo sasa
imesambaa katika kanda zote kutoa elimu kwa
viongozi wa Chadema.
“Katika kanda zote nchi nzima viongozi
watakwenda kuzungumza na wanachama wa kada
zote na kuwaelimisha kwanini Kamati Kuu imefikia
maamuzi ya kuanzisha Ukuta kabla ya kushiriki
mikutano na maandamano Septemba Mosi,”
alisema.chanzo mpekuzi blog
0 comments :
Post a Comment