Breaking News
Loading...

Advert

Wednesday, August 31, 2016

Polisi wapiga kambi ofsi cha CHADEMA.soma zaid

NI mwendo wa doria. Ndivyo unavyoweza
kusema baada ya askari polisi kulazimika kupiga
kambi katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
zilizopo Mtaa wa Ufipa, Dar es Salaam.
Polisi hao tangu jana asubuhi walikuwa
wakifanya doria katika eneo hilo huku wengine
wakizingira ofisi za chama hicho wakiwa
wamevaa kiraia.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilituma timu
ya waandishi ambao kutwa nzima ya jana
waliwashuhudia askari polisi wakiwa nje ya ofisi
za chama hicho na wengine wakiwa ndani ya
magari ya doria.
Hatua hiyo ilionekana kuzua taharuki kwa baadhi
ya wanachama na viongozi wa juu wa chama
hicho ambao walijikuta wakishindwa kufanya
kikao cha dharura cha Kamati Kuu kwa hofu ya
kuzuka vurugu.
Ilipotimu saa tano asubuhi, timu ya walinzi wa
Chadema ‘Red Brigade’ waliongezeka na
kusimama nje ya ofisi za makao makuu huku
wakionekana kuwa tayari kwa lolote, ikiwamo
kujihami kwa kuwalinda viongozi wao; mawaziri
wakuu wa zamani, Edward Lowassa na
Frederick Sumaye ambao waliwasili katika ofisi
hizo kwa ajili ya kikao.
Kikao hicho kilikuwa ni cha mwandelezo baada
ya kile cha juzi kushindwa kumalizika na baadhi
ya viongozi wa chama hicho kukamatwa na
polisi.
Pamoja na hali hiyo, ilipotimu saa 9 alasiri,
viongozi hao wakiongozwa na Lowassa walitoka
nje na kuelezwa kuwa kikao kimeshindwa
kufanyika kwa kuwa hali ya usalama si nzuri,
hasa baada ya kuonekana askari kanzu
wakiingia ndani ya ofisi hiyo na wengine
kujifanya ni wanachama wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
pamoja na Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji,
walilazimika kuondoka mapema na kwenda
katika kikao cha pamoja kati yao na viongozi wa
dini ili kutafuta mwafaka, kuhusu Operesheni
Ukuta inayotarajiwa kufanyika kesho licha ya
kuzuiwa na Jeshi la Polisi.
Kikao hicho cha viongozi wa dini kilichofanyika
katika Hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam,
pamoja na mambo mengine kilijadili kwa kina
mkwamo wa kutafuta suluhu kati ya viongozi wa
Chadema na Serikali kuhusu kuzuiwa
maandamano ya kesho.
MTANZANIA ilipomtafuta Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Mashinji ili kupata ufafanuzi
kuhusu kuzingirwa kwa ofisi zao na maofisa wa
polisi, alikiri kutokea kwa hali hiyo.
“Ni kweli tumeahirisha mkutano wetu wa Kamati
Kuu mpaka hapo baadaye, Ofisi zetu za Makao
makuu zilizingirwa na askari wa kila aina,
wengine walivaa baraghashia, kanzu na kila aina
ya nguo kwa lengo la kuvunja na kutawanya
mkutano wetu wa ndani, tumeuahirisha mpaka
wakati mwingine, tutawajulisha.
“Askari hao wamekuwa wakipiga kambi katika
ofisi zetu kwa muda wa wiki sasa, lakini kadiri
siku zinavyokwenda idadi yao inazidi kuongezeka
kama ilivyokuwa leo (jana),” alisema Dk.
Mashinji.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza
kuwa wajumbe wa Kamati Kuu walikutana ili
kujadili mambo mbalimbali ikiwamo suala la
maandamano yanayotarajiwa kufanyika nchi
nzima kuanzia kesho.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top