Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzani(JWTZ) mbaroni kwa kuiba mtoto.soma zaid
POLISI mkoani Tabora inamshikilia askari wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),kwa
tuhuma za kuiba mtoto mchanga,Razack
Kombo, mwenye umri wa miezi miwili.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata
jana na kudhibitishwa na Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Tabora,Khamis Issa, zinasema askari
huyo wa Kikosi cha Jeshi Mirambo, anashikiliwa
baada ya kichanga hicho kufariki dunia katika
mazingira ya kutatanisha.
“Tunamshikilia askari huyo tangu wiki iliyopita
kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga ambaye
pia alifariki dunia katika hali iliyojaa utata
ingawa bado tunaendelea kufanya mahojiano
naye ili atueleze namna hali ilivyokuwa.
“Hivi ninavyoongea na wewe niko nje ya
ofisi,lakini wasaidizi wangu wamenijulisha
wamemkamata.Haiingii akilini mtu aibe
kichanga hiki alafu kipoteze uhai ndani ya muda
mfupi, tena mwili wake umekutwa kwenye moja
ya hospitali ya jeshi,japokuwa taarifa
zinaonyesha alikuwa haumwi.
“Kama ningekuwa ofisini, ningeweza kukutajia
namba za askari huyo pamoja na majina kamili
kwa sababu tunayo.
“Lakini, nakuomba univumilie kama nitawahi
kurudi ofisini, tutawasiliana zaidi.
“Katika mahojiano ya awali, askari huyo alisema
alikuwa anakwenda likizo ya uzazi nyumbani
kwao,japo hakuwa na ujauzito.
“Inaonekana mama wa mtoto aitwaye Daphina
Matwika, alikuwa anasafiri kutoka Morogoro
kwenda Mpanda kule Katavi akiwa na watoto
wengine wakubwa wawili.
“Kwa hiyo, baada ya kutokea wizi huo, mama
wa mtoto alikwenda kutoa taarifa kituo cha
polisi cha stendi kuu ya mabasi Tabora ambapo
polisi walianza kuweka mitego iliyosaidia
kumnasa askari huyo,” alisema Kamanda Issa.
Baada ya kumkamata askari huyo, Kamanda
Issa alisema waliwasiliana na mama wa
marehemu ambaye tayari aliyekuwa amefika
Mpanda na aliporudi, alimtambua mtoto huyo.
“Baada ya utambuzi wa mwanamke huyo,
uliibuka mvutano kati yake na askari huyo kwani
kila mmoja alikuwa akidai mtoto ni wake.
“Tulichokifanya ni kuwafanyia kipimo cha
kuwachukua damu na kutuma vipimo hivyo kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema.
Mama asimulia
Akizungumza na MTANZANIA jana kutoka
Mpanda, mama wa marehemu alisema
ameumizwa na tukio hilo na sasa yupo katika
wakati mgumu.
“Nakumbuka Jumatatu wiki iliyopita nilipanda
basi la Kampuni ya NBS pale Msamvu
Morogoro, nikiwa na watoto wangu watatu
akiwamo marehemu nikielekea Mpanda.
“Safari yetu ilianza kupata matatizo tulipofika
Dodoma kwa sababu basi lilikamatwa na dereva
aliwekwa ndani karibu saa nne hivi kwa sababu
alipishana lugha na trafiki.
“Baadaye tuliondoka Dodoma kwenda Tabora
ambako tulifika saa 3:30 usiku.
“Wenye basi walituteremshia ofisini kwao
badala ya stendi. Kwa hiyo, nilichukua teksi
hadi stendi kuu ambapo nilitafuta nyumba ya
kulala wageni nikakosa.
“Tuliamua tulale pale pale stendi na wakati
wote huo, yule dada alikuwa pembeni yangu
ananiangalia tu.
“Ilipofika majira ya saa saba usiku, alinifuata
nilipokuwa nimelala akaniambia niinuke niende
alipo lala yeye kwa sababu ameweka mkeka,
lakini nilimkamtalia.
“Cha ajabu ilipofika saa 10 alfajiri, alikuja tena
akaniomba anisaidie kubembeleza mtoto kwa
sababu alikuwa analia, lakini pia nilikataa kisha
aliniambia twende uani, pia nikakataa.
“Nilipomkatalia, aliondoka kisha
akarudi,akaniomba tena mtoto nikamkatalia na
wakati huo nikamkabidhi mwanangu mkubwa
yule mtoto mimi nikaenda uani.
“Inaonekana nilipokwenda uani tu, alimwambia
mwanangu mkubwa wasogee mbele, ghafla
akamwambia arudi aangalie mabegi yasiibiwe
huku akiwa na mtoto, sasa aliporudi ndiyo
akatoroka pale na yule mwanangu
mdogo,”alisema Daphina.
Baada ya tukio hilo, alisema alipiga kelele
kuomba msaada na baadaye akaambiwa akatoe
taarifa polisi kwa msaaad zaidi.
” Nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kutoka
kwa askari kwani walinisaidia kumpata
mtuhumiwa pamoja na mwili wa marehemu
mwanangu uliokuwa umehifadhiwa katika
Hospitali ya Jeshi Mirambo,” alisema.
Source: Mtanzania
0 comments :
Post a Comment