Ndoto ya Davidi Kafulila kurudi Bungeni katika kipindi hiki cha miaka mitano zimegonga Mwamba.soma zaid
Hatimaye mbio za David Kafulila kupinga
mahakamani matokeo ya uchaguzi wa ubunge
wa Kigoma Kusini ya Oktoba mwaka jana
uliompa ushindi Husna Mwilima (CCM) zimefika
ukingongoni baada ya mahakama ya rufaa
kutupilia mbali maombi yake.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa
waliokaa mjini Tabora, jana lilitoa maamuzi yake
kuhusu rufaa ya Kafulila na kueleza kuwa
wameyatupilia mbali maombi hayo kwakuwa
yamekosa nguvu yenye uhalali wa Kisheria.
Aidha, Mahakama hiyo ya Rufaa imemtaka
Kafulila ambaye hakuhudhuria mahakamani
hapo, kulipa gharama zote za shauri hilo la
madai namba 212 la mwaka 2016.
Akizungumza baada ya maamuzi hayo ya
Mahakama ya Rufaa, Mbunge wa Kigoma Kusini,
Mwilima alisema Kafulila alijua kuwa hakuwa na
madai yoyote mahakamani na kwamba
alicholenga ni kumsumbua ili akose muda wa
kuwatumikia wananchi wake.
“Kafulila alijua fika kuwa hakuna kesi ya yeye
kukata rufaa. Lakini alikata rufaa kunisumbua ili
nikose muda wa kuwatumikia wananchi
waliniingiza bungeni,” alisema Mwilima.
Kafulila alifungua shauri la madai namba 2 la
mwaka 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya
Tabora, akipinga ushindi wa Mwilima. Katika
shauri hilo, Kafulila aliwalalamikia Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa uchaguzi na
Husna Mwilima.
Mahakama Kuu iliyatupilia mbali maombi ya
Kafulila ya kutaka kutengua ubunge wa Mwilima
ndipo Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma
Kusini alipoamua kukata rufaa katika Mahakama
ya Rufaa ambayo ni Mahakama ya juu zaidi
nchini.
Kesi hiyo iliyovuta umakini wa wananchi wengi
jimboni humo na huenda ndio kesi ya uchaguzi
iliyovuta watu wengi zaidi tangu kumalizika kwa
uchaguzi wa mwaka jana, imefikia ukingoni kwa
kuhalalisha ubunge wa Mwilima.
0 comments :
Post a Comment