Rais magufuli amuelezea kenyatta kuwa watanzania wanapiga kazi.
RAIS John Magufuli ametua Kenya na kumweleza
mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta na
wananchi wa Kenya kwamba Serikali ya Awamu
ya Tano inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili
nchi isonge mbele huku akisisitiza ‘Hapa Kazi Tu’
katika ulipaji kodi na kukabiliana na ufisadi.
Aidha, alisema Kenya ni nchi inayoongoza kwa
uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi
nyingine za Bara la Afrika. Rais Magufuli
aliyasema hayo jana katika mkutano na
waandishi wa habari, uliofanyika katika Ikulu ya
Nairobi nchini Kenya ambako ameanza ziara ya
kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais
Kenyatta.
“Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii ili nchi
iende mbele. Tunasisitiza Watanzania walipe kodi
na tunakabiliana na ufisadi,” alisema Rais
Magufuli na kuitaka Tume ya Pamoja ya
Mawaziri wa Mambo ya Nje kukutana haraka ili
kukamilisha taratibu za ushirikiano kwa sababu
imechukua miaka minne sasa.
“Kule nchini nina msemo wangu kwamba ‘Hapa
Kazi Tu’, hivyo lazima tufanye hili kwa haraka ili
tusonge mbele kwa sababu tumekuwa
tukizungumza kwa miaka minne sasa,” alisema
Rais Magufuli mbele ya wenyeji wake, Rais
Kenyatta na maofisa wa nchi hizo mbili.
Akizungumzia uwekezaji, Rais Magufuli ambaye
kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari,
alipokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na
kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa
heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo
rasmi na mwenyeji wake, alisema takwimu za
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha
kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529
zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania,
ambapo zimewekeza Dola za Marekani bilioni 1.7
na zimeajiri watu 56,260.
Pia, Rais Magufuli amebainisha kuwa biashara
kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka
Sh za Kitanzania bilioni 652.9 hadi Sh trilioni
2.044.
"Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na
ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa
mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio
nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote
za Afrika.
"Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu
wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu
ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila
siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka
katika nchi zote mbili bila kujali mipaka,” alisema
Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dk Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake
itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na
Kenya, ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa
Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa
Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na
aliwakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa
Kenya kuwekeza nchini.
"Kabla ya kuja hapa nimekwenda kutoa heshima
katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli
nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na
wazee wetu, naomba niwahakikishie kuwa
tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na
tutaendelea kufanya hivyo,” alisisitiza Dk
Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alimshukuru
Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na
alimhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na
kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na
Tanzania.
"Kwetu sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na
dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa
kidugu na tutahakikisha tunauendeleza
ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na
wazee wetu,” alisema Uhuru.
Rais Uhuru alisema Tanzania na Kenya ni nchi
zinazofanana kwa mambo mengi muhimu,
ikiwemo kubadilishana uongozi wa serikali kwa
njia ya amani na aliongeza kuwa katika
mazungumzo yao, wamekubaliana kuwa nchi hizi
zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika
Mashariki, zinazokabiliwa na matatizo
mbalimbali.
Aidha, alisema Kenya itaendelea kushirikiana na
Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano,
ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile
barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi
(Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo
Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizi
mbili itayaainisha.
Jana jioni, Rais Magufuli alitarajiwa kuhudhuria
dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi,
aliyoandaliwa na mwenyeji wake na leo
anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha
Eldoville kilichopo Karen jijini Nairobi, na kuzindua
barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo
jijini humo. Hii ni ziara ya tatu nje ya nchi kwa
Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwaka
mmoja sasa. Ziara nyingine alikwenda Rwanda
na nyingine Uganda.
0 comments :
Post a Comment