Serikali kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi wote wa umma.soma zaid
SERIKALI imeahidi kuboresha na kuimarisha
maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia
Bodi ya Mishahara na motisha mara
watakapokamilisha uhakiki wa taarifa za
kiutumishi kwa wafanyakazi wa umma, ambao
utawezesha kupanga upya mishahara na motisha
kwa watumishi.
Aidha, imesema italipa madeni yote inayodaiwa
na watumishi wake wote mara itakapomaliza
kufanya uhakiki huo ili kubaini watumishi hewa.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya
miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(Udsm).
Katika hotuba yake, Majaliwa alisema Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha
inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi
wote wa umma, na mojawapo ya mikakati hiyo ni
uhakiki, ambao unaendelea wa watumishi wa
umma. Alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu
watumishi hewa, ambao wamebainika kutokana
na uhakiki huo walikuwa ni 16,500.
“Baada ya uhakiki huo tutarudia uhakiki wa
madeni yote yaliyowasilishwa serikalini na kisha
tutalipa madeni ya watumishi wote yakiwemo
madeni yanayodaiwa na wanataaluma,” alisema
Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa muda mrefu sasa, serikali inaendesha
uhakiki wa watumishi wa umma baada ya
kubainika kuwapo na watumishi hewa wengi
wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi, hivyo
kuipotezea mapato serikali ambayo yangetumika
kwa kazi nyingine, zikiwamo za kuboresha
mishahara ya watumishi na huduma za kijamii.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili Chuo
Kikuu cha Dar es Salam likiwemo suala la uhaba
wa wahadhiri waandamizi pamoja na tatizo la
mikopo kwa wanafunzi, Majaliwa alisema serikali
itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji
wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo.
Lakini, pia amevitaka vyuo vya umma,
kuhakikisha taratibu na mipango endelevu ya
kurithishana kwani bila kufanya hivyo wakati
wote kutakuwa na mapungufu katika utoaji wa
taaluma. Alisema serikali itaendelea kuwaajiri
wanataaluma na watumishi wengine wapya pale
wanapohitajika.
Alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Makamu
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza
Mukandala kuwa chuo hicho kwa sasa
kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahadhiri
waandamizi kutokana na wengi wao kustaafu.
Kuhusu changamoto ya mikopo ya wanafunzi wa
elimu ya juu, Majaliwa alisema Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za
waombaji wa mikopo na akasema kufikia kesho
asilimia 90 ya waombaji ambao wametimiza
masharti watakuwa wameshalipwa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutimiza wajibu wao
kuhakikisha kwamba, kwa wale ambao uhakiki
wao umekamilika wapatiwe mikopo hiyo kwa
wakati. Alisema kamwe serikali haitawavumilia
watumishi ambao watachelewesha kwa makusudi
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kama kuna taarifa itolewe ndani ya serikali
haraka ili ifanyiwe kazi kuzuia mgogoro kati ya
wanafunzi na serikali yao,” alisema Majaliwa.
Awali, Profesa Mukanda alisema changamoto
kubwa inayokikabili chuo hicho kwa sasa ni
uhaba wa wanataaluma waandamizi katika fani
mbalimbali tatizo ambalo alisema linatokana na
serikali kusitisha ajira kwa miaka 10 na hivyo
kutoajiriwa wanataaluma chipukizi.
Alisema hali ilivyo kwa sasa katika vyuo vya
umma nchini ni mamia ya wanataaluma wazoefu
kustaafu kwa wakati mmoja na wanataaluma
walioajiriwa katika miaka ya hivi karibuni, bado
wako masomoni au wangali chipukizi katika
taaluma zao na hivyo kutokuwa na uwezo wa
kutosha kubeba majukumu ya kufundisha
shahada za umahiri na uzamivu.
Alisema licha ya serikali kuruhusu utoaji wa ajira
za mikataba kwa wanataaluma wanaostaafu,
lakini bado idara nyingi zinakabiliwa na uhaba
mkubwa wa wanataaluma waandamizi.
Alisema hali hiyo inatishia kukwamisha
utekelezaji wa azma na mpango mkakati wa
chuo hicho ambao ni kupanua programu za
mafunzo ya digrii katika ngazi za umahiri na
uzamivu.
Kwa hali hiyo aliiomba serikali kutoa mwongozo
utakaosaidia vyuo vikuu vya umma
vinavyokabiliwa na changamoto hiyo ili viweze
kuepuka hatari iliyopo ya kushuka kwa viwango
ya utoaji maarifa.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiko tayari kutoa
mchango wa mawazo kuhusu namna ya kuruka
kizingiti hicho,” alieleza.chanzo habar leo
0 comments :
Post a Comment