Wafuasi 22 wa kundi la Blue Guard la chama cha CUF wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.soma zaid
WAFUASI 22 wa Kundi la ‘Blue Guard’ la Chama
cha Wananchi (CUF) wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne
likiwemo la kukutwa na silaha za Jeshi la Polisi.
Washitakiwa hao ambao ni wakazi wa Zanzibar
walifikishwa mahakamani hapo jana na
kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali,
Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey
Mwambapa.
Mwita alidai, washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka manne ya kula njama, kuingilia
majukumu ya kipolisi kupitia genge la uhalifu
pamoja na kukutwa na silaha pamoja na zana za
Jeshi la Polisi.
Akisoma mashitaka, Wakili Mwita alidai, kati ya
Septemba 20 na 25, mwaka huu kati ya Zanzibar
na Dar es Salaam, kupitia kikundi cha Blue
Guard, washitakiwa na wenzao ambao
hawakufikishwa mahakamani walikula njama za
kuajiri watu, wafanye kazi za kipolisi kinyume cha
Sheria ya Makosa ya Jinai.
Aliendelea kudai kuwa, washitakiwa wakiwa
wanachama wa kundi la Blue Guard waliwaajiri
watu kwa ajili ya kufanya kazi za Kipolisi
kinyume na sheria.
Wakili Mwita alidai, Septemba 25, mwaka huu
katika eneo la Mwananyamala, Dar es Salaam,
wakiwa na lengo la kutenda kosa, washitakiwa
walikutwa wakiwa na silaha kinyume cha sheria ,
ikiwemo visu vitano pamoja na mabomu ya
machozi 10 kwa ajili ya kuyatumia katika
uvamizi.
Aidha, inadaiwa siku hiyo hiyo, Dar es Salaam,
washtakiwa walikutwa wakiwa na zana za Jeshi
la Polisi ambazo ni mabomu ya machozi
yanayotumiwa na jeshi hilo katika majukumu yao.
Baada ya kusomewa mashitaka washitakiwa hao
walikana kutenda makosa hayo, hata hivyo Wakili
Mwita alidai upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe
nyingine ya kutajwa.
Upande wa utetezi kupitia Wakili Hekima
Mwesigwa uliiomba Mahakama kuliondoa shitaka
la tatu katika makosa hayo kwa sababu lina
upungufu wa kisheria kwa kutumia baadhi ya
maneno kupotosha.
Hata hivyo, Wakili Mwita aliiomba Mahakama
kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa shitaka
hilo halina upungufu wowote badala yake
wametumia lugha ya mkato.
Hakimu Mwambapa alisema baada ya kupitia
vifungu vya sheria, amebaini kuwa shitaka halina
mapungufu kisheria hivyo ametupilia mbali
maombi.
Aidha, alisema washtakiwa hao watapata
dhamana endapo watatimiza masharti ya kuwa
na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini
hati ya Sh milioni mbili kila mmoja, pia
wawasilishe vitambulisho vyao mahakamani. Kesi
itatajwa tena Oktoba 20 mwaka huu.
Washtakiwa ni Hamis Omary Said (49), Said
Mohamed Zaharan (57), Hamid Nassor Hemed
(44), Nassor humud Ally (25), Othman Humud
Abdlaah (34), Swalehe Ally Swalehe (30), Hamis
Hamis Haji (46), Majid Hamis Juma (58),
Mohamed Hamis Ally (34), Ramadhan Rashid
Juma (30), Juma Hamad Seif (21) na Masoud
Iliyasa Fumu (29).
Wengine ni Jecha Faki Juma (40), Mbaruku
Hamis Bakari (31, Mohamed Alli Zuberi (43),
Muhsin Ally Juma (27), Mohamed Amir Mohamed
(30), Ally Juma Salum (35), Juma Hajji Mmanga
(26), Ally Nassoro Ally (46), Haji Rashid Juma
(32) na Juma Omary Hamis (28).
Kufikishwa mahakamani kwa washtakiwa hao
kunatokana na mgogoro unaoendelea ndani ya
chama hicho. Septemba 28, mwaka huu,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro alitoa taarifa za kukamatwa
kwa wafuasi hao kwa tuhuma za kupanga njama
za kufanya fujo na kuchoma ofisi za CUF zilizopo
Buguruni Ilala jijini Dar es Salaam.
0 comments :
Post a Comment