Ndege yaanguka ikiwa na watu 47 huko Pakistani.soma zaid
Islamabad, Pakistan. Ndege ya Shirika la
Pakistan imeripotiwa kuanguka kaskazini mwa
nchi hiyo ikiwa na abiria 47 muda mfupi baada
ya kuanza kuruka.
Taarifa za maofisa wa polisi zimesema kuwa
ndege hiyo yenye namba PK-661 iliyokuwa
ikiruka kutoka mji wa Chitral kuelekea Islamabad
ilipoteza mawasiliano kabla ya baadaye
kudhibitishwa kuwa ilikua imeanguka.
Msemaji wa shirika hilo, Danyal Gilani alisema
ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 30 na wengine
waliosalia wakiwa wahudumu na marubani.
Katika taarifa yake shirika hilo lilisema ndege
hiyo ilikuwa imebeba watu ‘wanaokadiriwa kuwa
40’ lakini taarifa kutoka mamlaka ya anga ilisema
kulikuwa na watu 47. Ofisa mwandamizi wa
polisi, Laiq Shah alisema ndege hiyo ilianguka
katika eneo linalofahamika kama Haveliana.
“ Timu ya waokoaji imeelekea kwenye eneo la
tukio nadhani baada ya hapo tutapata taarifa
zaidi,” alisikika akieleza msemaji wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege, Pervez George wakati
akizungumza na Reuters.
Maofisa wa polisi katika eneo hilo waliiambia
televisheni ya taifa kuwa ndege hiyo ilianguka
katika kijiji kimoja kilichopo kaskazini mashariki
mwa Pakistan.
Shirika la habari la AP liliarifu kuhusu kundi la
waokoaji kuelekea kwenye eneo la tukio. Moshi
mkubwa ulishuhudiwa ukivuka toka eneo ambalo
ndege hiyo ilianguka. Imeelezwa kuwa ndege
hiyo ilipoteza mawasiliano dakika 90 tangu ianze
kuruka.
0 comments :
Post a Comment