Breaking News
Loading...

Advert

Thursday, April 14, 2016

Mafisad wa NSSF sasa tumbo joto ripoti ya (CAG)yafika kwa raisi.soma zaid.

Patricia Kimelemeta na Christina Gauluhanga
RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) inayohusu miradi inayosimamiwa
na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),
imepelekwa kwa Rais Dk. John Magufuli kwa ajili
ya kuipitia.
Awali ripoti hiyo ilitakiwa kuwasilishwa juzi
kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge,
baada ya wajumbe wa kamati hiyo kuiomba,
lakini ilishindwa kuwasilishwa na viongozi wa
NSSF kwa madai kuwa kuna tuhuma za
ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi
mbalimbali inayosimamiwa mfuko huo.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo juzi,
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Jenister Mhagama, aliwaambia ripoti
hiyo imetua mikononi mwa Rais Magufuli, hivyo
hawawezi kuipata hadi aisome na kuiwasilisha
bungeni.
“Kutokana na hali hii, kamati haiwezi kuipata
ripoti hii hadi rais mwenyewe atakapoamua
kuiwasilisha,” alisema.
Alisema kuna uwezekano mkubwa mjadala wa
ripoti hiyo ukaendelea bungeni, baada ya Rais
Magufuli kuipitia na kutoa maelekezo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kamati hiyo
viliiambia jana kuwa baada ya
Waziri Jenister kutoa taarifa hiyo, wajumbe wa
kamati walipinga na kuwataka watendaji wa
NSSF waiwasilishe kwenye kamati hiyo kwa
sababu wao ndio walioiomba ili waweze kuipitia
na kuangalia utekelezaji wa majukumu ya mfuko
huo.
Baada ya mvutano huo, Waziri Jenister alisisitiza
taarifa alizonazo ripoti ipo kwa Rais, hivyo
hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuipata hadi
ipelekwe bungeni au atoe maelekezo mengine
kwa kuwa yeye ndie mwenye kibali hicho kwa
mujibu wa sheria.
Waziri Jenister alipotafutwa na
kuzungumzia suala hilo jana, alisema wizara yake
haiwezi kulizungumzia kwa sababu liko mikononi
mwa kamati.
Alisema kisheria ripoti ikifikishwa kwenye mikono
ya rais, wizara haina mamlaka ya kujadili tena.
Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Mohammed Mchengerwa, wakati akitoa
majumuisho ya ziara walizofanya katika taasisi
mbalimbali za Serikali na wizara, alisema
walibaini kuwapo upungufu katika taarifa ya
utekelezaji wa miradi mingi inayosimamiwa na
NSSF.
Alisema kutokana na kasoro hizo, kamati iliona ni
vema ikapata ripoti ya CAG ili ipitie na
kujiridhisha kama miradi imetekelezwa au kuna
harufu ya ufisadi.
“Kamati imebaini kuwepo nyumba nyingi
zilizojengwa na NSSF ambazo hazikaliwi na watu,
hali iliyotutia shaka. Inaonekana baadhi ya watu
wamenufaika na miradi hii.
“Tunaamini miradi hii haijawanufaisha
wanachama wake bali watu wachache, ndiyo
maana tumeagiza ripoti ili tuipitie,” alisema
Mchengerwa.
Alisema kutokana na hali hiyo, wameagiza
kusimamishwa miradi mipya ya shirika hilo na
kuiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya
Jamii (SSRA), kuhakikisha inasimamia ipasavyo
mifuko pamoja na kuangalia miradi
inayoanzishwa kama inawanufaisha wananchi na
Serikali kwa ujumla.chanzo mtanzania

0 comments :

Post a Comment

Back To Top