Denmark na Tanzania kujenga kiwanda cha mbolea wilayani kilwa mkoani lindi
Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa kiwanda
kikubwa cha kuzalisha mbolea kabla ya mwisho
wa mwaka huu wa 2016 katika wilaya ya Kilwa
Mkoani Lindi.
Kiwanda hicho ambacho kitatumia rasilimali ya
gesi asili na miamba ya matumbawe (coral
reefs) iliyopo wilayani Kilwa, kitajengwa kwa ubia
kati ya Tanzania na nchi za Denmark, Ujerumani
na Pakistani na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha
tani 3,800 za mbolea kwa siku.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Egon
Kochanke na Balozi wa Denmark hapa nchini
Mheshimiwa Eina Hebogrd waliokutana na
kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli leo tarehe 19 Mei, Ikulu Jijini Dar es
salaam, wamesema kiwanda hicho kikubwa
barani Afrika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha
mbolea nyingi itakayotosheleza mahitaji ya
wakulima wa Tanzania na nyingine kuuzwa nje
ya nchi.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha ajira zaidi
ya 5,000 na uwekezaji wake utagharimu dola za
kimarekani Bilioni 3.
Pamoja na kuwahakikishia kuimarishwa kwa
uhusiano na ushirikiano kati ya serikali yake na
nchi za Ujerumani na Denmark, Rais Magufuli
amewaahidi mabalozi wanaowakilisha nchi hizo
hapa nchini kuwa serikali yake ya awamu ya tano
itatoa ushirikiano wa kutosha kuharakisha
utekelezaji wa mradi huu mkubwa na
amependekeza mchakato wa ujenzi uanze na
kukamilishwa haraka.
Aidha, Rais Magufuli na Mabalozi hao
wamezungumzia maeneo mengine ya ushirikiano
kati ya nchi hizo na Tanzania ikiwemo kukuza
biashara na uwekezaji, kuendeleza bandari za
Tanzania na kuimarisha mapambano dhidi ya
rushwa.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amezungumza na
Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Yasemin
Eralp ambapo pamoja na kukubaliana kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi
mbili, ameikaribisha nchi hiyo kuwekeza hapa
Tanzania katika uzalishaji wa dawa za kutibu
binadamu na kujenga viwanda vya kuzalisha
bidhaa mbalimbali kutokana na nchi hiyo
kubobea katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amekutana na Katibu Mtendaji wa
Jumuiya ya nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la
Sahara (SADC) Dkt. Stergomena Tax na
kuzungumzia hali ya ulinzi na usalama katika
Jumuiya hiyo.
Rais Magufuli ambaye kuanzia mwezi Agosti
mwaka huu 2016 atakuwa mwenyekiti wa Taasisi
ya Ulinzi, Usalama na Siasa iliyo chini ya SADC
amesema pamoja na majukumu mengine ya
Jumuiya hiyo ni muhimu kwa sasa kujikita zaidi
katika uchumi na maendeleo ya wananchi
hususani ujenzi wa viwanda.
Kwa upande wake Dkt. Stergomena Tax
ameungana na Rais Magufuli kuwasihi
watanzania na wanajumuiya wote wa SADC
kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo katika
kilimo, masoko, viwanda na ajira ndani na nje ya
jumuiya.
0 comments :
Post a Comment