Breaking News
Loading...

Advert

Monday, May 9, 2016

Marufuku viongozi kujihusisha na biashara.soma zaid.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametaja
sababu zinazochochea wabunge
kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa,
ni presha kutoka kwa wananchi
inayotokana na kutakiwa kuchangia
masuala mbalimbali katika majimbo yao.
Spika huyo pia amewatangazia rasmi
wabunge kuwa Ofisi ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia
kuwasilisha bungeni muswada wa sheria
utakaotenganisha uongozi na biashara.
Aliyasema hayo wakati akizungumza
katika uzinduzi wa Chama cha Wabunge
wanaopambana na Rushwa (APNAC),
mjini hapa. Aliwataka wabunge hao
kujiepusha na vitendo vya rushwa licha
ya kuwa na maslahi madogo.
Pia aliwataka wajiandae na sheria hiyo
kutokana na ukweli kuwa katika bunge
hilo wabunge wengi pia ni
wafanyabiashara. Presha za rushwa
Alitaja sababu za wabunge wa Tanzania
kujiingiza kwenye rushwa ni presha za
wananchi wao kuwataka wachangie kila
inapotokea msiba, sherehe, madawati,
madarasa, barabara hadi ada.
Alisema kutokana na kipato kidogo cha
fedha, wabunge wengi hutafuta mbinu
mbadala za kupata fedha kumudu
gharama hizo. Mishahara ya wabunge
na marupurupu yake kwa mwezi
yanakadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni
11 kwa mwezi.
Sababu nyingine ni mikopo yenye riba
kubwa ambayo wabunge wengi
wameichukua ikiwa ni pamoja na
maslahi madogo wanayopata wabunge
hao. “Kutokana na hali hii wakati
mwingine humfanya kiongozi ahangaike
kutafuta fedha na ndipo wengine
hujiingiza katika vitendo hivi vya
rushwa.
Nawatahadharisha ninyi kama wabunge
mnao wajibu wa kudhibiti rushwa na
kuwa mfano katika jamii,” alisema.
Spika alilia maslahi Alisema katika eneo
la maslahi, ofisi ya Bunge inatambua
kuwa bado maslahi wanayopata
wabunge hao ikilinganishwa na kazi
wanayofanya ni madogo hivyo,
wanaendelea kuangalia namna ya
kuyaboresha.
Ndugai alisema wabunge wa Tanzania
wana wajibu na jukumu kubwa la
kudhibiti rushwa kwa kutunga sheria
zinazopaswa kutumika katika kuunga
mkono au kuleta miswada itakayosaidia
kutokomeza rushwa. Alisema pia moja
ya kazi ya wabunge ni kushauri na
kusimamia Serikali.
Alisema ni vyema pale ambapo kuna
viashiria vya rushwa wakatoa ushauri
huo bila kukubali kushawishiwa kwa
rushwa. “Vilevile katika kupitisha bajeti
za serikali, hapana budi kuhakikisha
vyombo vinavyohusika na mapambano
dhidi ya rushwa vimetengewa fedha za
kutosha,” alisema.
Aliwaasa wabunge kujiepusha na
vishawishi vya rushwa kwa kuwa nafasi
waliyonayo ni nyeti. Alisema pia
kutokana na mwenendo wa umakini wa
Serikali ya Awamu ya Tano,
inawezekana wakawepo watu wanaoona
umakini huo kama maslahi yao na
kutumia njia pekee ya kuwarubuni
wabunge.
“Nawaasa msishawishike,” alisisitiza.
Alisema kwa mujibu wa Jumuiya ya
Vyama vya Wabunge Wanaopambana na
Rushwa Afrika (GOPAC), takribani dola
za Marekani bilioni 50 hutoroshwa
Afrika kutokana na rushwa. “Hizi ni
fedha nyingi sana za walalahoi
zinazotumika kwa maslahi ya
wachache,” alisema.
Pia amehamasisha wabunge hao
kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa
kile alichosema, katika awamu hii ya
serikali ya awamu ya tano, yeyote
atakayebainika kujihusisha na vitendo
hivyo lazima aingie matatani. Sheria ya
maadili “Muda si mrefu nitawaalika
waje watoe semina kwenu kuhusu
undani wa sheria hiyo ili wote muielewe
vyema.
Nawashauri muisome vizuri sheria hii
ikija kwa sababu wengi wetu pamoja na
ubunge tunafanya biashara ili
tujiendeshe vizuri,” alisisitiza Ndugai.
Alisema sheria hiyo ikipitishwa,
haitakuwa ya kwanza Tanzania
kuitekeleza kwani nchi nyingi duniani
zimekuwa na mfumo unaotenganisha
viongozi wake na biashara.
“Wenzetu ni kawaida ukiingia kwenye
siasa unakabidhi biashara yako mpaka
pale utakapomaliza uongozi wako ndio
unaruhusiwa kuendelea, naomba
mjiandae kuipokea sheria hii, ni sheria
nzuri na ina malengo mazuri,” alisema.
Akizungumzia rushwa, alisema kila
bunge lina sababu zake za wabunge
kujiingiza katika vitendo vya rushwa .
Wabunge; sheria hiyo ni mwiba Baadhi
ya wabunge waliozungumza na gazeti
hili baada ya mkutano huo kumalizika,
walisema sheria itakayotenganisha
viongozi na biashara ni mwiba kwa
wabunge wengi na itakapowasilishwa
bungeni itazua tafrani.
“Sikufichi, wabunge wengi sisi hapa
mnavyotuona ni wafanyabiashara,
ukituvua tu nafasi ya biashara hatuna
kitu, hili kwa kweli kwetu ni mtihani
haya tusubiri tuone,” alisema mmoja wa
wabunge hao aliyekataa kutaja jina lake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi na Utawala
Bora, Angela Kairuki, aliwataka wabunge
kujiepusha kuhusishwa na rushwa
akisisitiza kwamba, kutokana na nafasi
yao katika jamii, wanapaswa kuwa
mstari wa mbele kudhibiti tatizo hilo na
kuwa mfano mbele ya jamii hiyo.
“Niwaambie ukweli kwa nafasi hii
tuliyonayo wabunge wenzetu hatutakiwi
hata kutuhumiwa kwa rushwa. Sisi ndio
tunatakiwa kuwa mstari wa mbele
kupambana kwa vitendo na walarushwa
nchini mwetu,” alisema.
Aidha alizungumzia suala la malalamiko
ya adhabu kwa walarushwa kuwa ndogo
na kukiri kwamba adhabu zinazotolewa
kwa watu wanaothibitika kufanya
vitendo vya rushwa ni ndogo
ikilinganishwa na hasara iliyotokana na
rushwa hiyo.
“Nawaahidi hili tumelipokea la adhabu
na tutawasilisha mapendekezo kwa ajili
ya kuifanyia kazi sheria yetu ya rushwa.
Naomba wabunge wenzangu mtuunge
mkono kwa hili,” alisema Waziri
Kairuki.
APNAC yapongeza kupunguza rushwa
Akiwasilisha mada ya kuhusu tathmini
ya shughuli za APNAC katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita, Mhadhiri wa
Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), Davis Mwamfupe, alisema
chama hicho kimefanikiwa kwa kiasi
kikubwa kueneza uelewa wa tatizo la
rushwa hususan kwa wabunge.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa
iliyopo katika kutatua tatizo la rushwa,
ni kutokana na mara zote rushwa
kufanyika kwa siri na hufanywa na
watu wenye nafasi kubwa katika jamii
wakiwemo wanasiasa na wachumi hivyo
kuwa vigumu kuwakamata.
Aliwataka wabunge hao kutotumia nafasi
zao ndani ya Bunge na kukemea rushwa
kwa mdomo pekee bali waoneshe
dhahiri kuichukia na kupambana nayo
kwa vitendo. Mbunge wa Nkasi, Ally
Keissy, wakati akichangia mada hiyo ya
rushwa, alisema tatizo la rushwa
litamalizika endapo Mahakama na
vyombo vya dola vitachunguzwa
kutokana na ukweli kuwa kesi nyingi za
rushwa zimefunguliwa, lakini
hazishindi.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top