Kigoma inashika nafasi ya kwanza kwa umasikini.soma zaid.
Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango amewasilisha bungeni Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa Fedha wa
2016/17, huku akitaja mikoa mitano inayoongoza
kwa umaskini nchini.
Dk Mpango alisema mikoa hiyo imebainika katika
Tathimini ya Hali ya Umaskini kimaeneo
iliyofanyika kwa kutumia takwimu za Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2012 na utafiti wa
Hali ya Kipato na Matumizi katika kaya ya
mwaka 2012.
Aliitaja mikoa hiyo na asilimia ya umaskini
kwenye mabano Kigoma (48.9), Geita (43.7),
Kagera (39.3), Singida (38.2) na Mwanza (35.3).
Kwa upande wa wilaya umaskini mkubwa upo
katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma na
Biharamulo mkoani Kagera na takribani asilimia
60 ya watu wapo chini ya mstari wa umaskini wa
mahitaji ya kimsingi.
“Hii ina maana kuwa maeneo ya vijijini hususan
pembezoni bado Watanzania wengi wanaishi
kwenye umaskini na uwezo wao wa kupata
mahitaji ya msingi mdogo,” alisema.
Dk Mpango aliitaja mikoa mitano yenye ahueni ya
umaskini wa kipato kuwa ni Dar es Salaam (5.2),
Kilimanjaro (14.3), Arusha (14.7), Pwani (14.7)
na Manyara (18.3).
Pia, Dk Mpango alisema utafiti wa Hali ya Afya
ya Mama na Mtoto, uliofanyika mwaka 2015
unaonyesha idadi ya wasichana waliopata watoto
katika umri wa miaka 15 hadi 19 imeongezeka na
kufikia asilimia 27 mwaka 2015 kutoka asilimia
23 mwaka 2010.
“Kuongezeka kwa wasichana wanaopata watoto
wakiwa na umri mdogo, yaani miaka 15 hadi 19
siyo dalili nzuri kwani inaashiria kuongezeka kwa
utegemezi na kudumaza jitihada za kuondoa
umaskini katika jamii,” alisema.
Kuhusu wastani wa pato la kila mtu, Dk Mpango
alisema pato la wastani la mtu limepungua
kutoka Dola 1,047 za Marekani kwa mwaka 2014
hadi Dola 966.5 mwaka 2015.
Alisema hali hiyo imetokana na kushuka kwa
thamani ya shilingi ya Tanzania. “Hivyo ni dhahiri
kuwa bado kunahitajika msukumo zaidi wa
kuongeza ukuaji wa Pato la Taifa ili kufikia
malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya
kufikia Dola 3,000 za Marekani kwa pato la kila
mtu na kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati
ifikapo mwaka 2025,” alisema.
Kuhusu urahisi wa kibiashara, Dk Mipango
alisema taarifa ya urahisi wa kufanya biashara
ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2015 ,
Tanzania ilipanda kwa nafasi moja katika vigezo
vya urahisi wa kufanya biashara kwa kushika
nafasi ya 139 kati ya nchi 189 duniani
ikilinganishwa na nafasi ya 140 mwaka 2014.
Alisema mwaka wa fedha 2016/17, Serikali
imetenga Sh11.8 trilioni sawa na asilimia 40 ya
bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
0 comments :
Post a Comment