Marekebisho Sheria ya manunuzi iwaacha njaa waliozoea upigaji dili.soma zaid.
MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya
Manunuzi wa Mwaka 2016, umesomwa kwa mara
ya kwanza bungeni jana na kuwekwa wazi kwa
umma, na moja ya vifungu vinavyopendekezwa ni
kuzuia mtu yeyote aliyewahi kuhukumiwa kwa
rushwa, kufanya biashara na serikali.
Katika marekebisho hayo yanayopendekezwa na
serikali, wizara, taasisi au shirika lolote la serikali
wakati wa kufanya biashara na kampuni yoyote,
ikibaini kampuni husika au mmoja wa
wakurugenzi wake aliwahi kuhukumiwa kwa
rushwa, biashara hiyo itasitishwa mara moja na
taarifa kutolewa serikalini.
Mbali na watu waliohukumiwa kwa makosa ya
rushwa, marekebisho hayo yamependekeza kuwa
pamoja na sifa nyingine za viongozi wakuu wa
serikali hasa maofisa watendaji wakuu,
watapaswa kuwa na sifa ya ziada ya uzoefu
katika masuala ya manunuzi.
Katika kukidhi haja ya kuondoa malalamiko ya
sheria iliyopo kutumika kuibia nchi, marekebisho
hayo yamesisitiza bei za huduma na bidhaa
zitakazotolewa ziwe za soko, ununuzi ufanyike
moja kwa moja kiwandani badala ya kupitia kwa
mtu wa kati na mkataba wa manunuzi, lazima
usainiwe mbele ya mashuhuda.
Watuhumiwa wa rushwa
Katika Ibara ya 83 ya Sheria hiyo,
imependekezwa ibara ndogo ya pili kwamba
shirika au wizara itakaporidhika kwamba kampuni
au mtu anayependekezwa kupewa zabuni,
amewahi kutangazwa na Mahakama kuwa
alishiriki katika vitendo vya rushwa, ufisadi, au
ukiukwaji wa taratibu wakati wa kushindania
zabuni, ofisi hiyo ya umma itapaswa kukataa
pendekezo la kumpa mhusika zabuni hiyo.
Ofisi hiyo ya umma, pia itapaswa kumtangaza
mtu huyo au mzabuni ikiwa ni pamoja na
wakurugenzi wake, kuwa hawapaswi kupewa
zabuni yoyote inayogharimiwa na fedha za
umma.
Pia ofisi hiyo ya umma, itapaswa kumtaka huyo
mtu au mzabuni, kurejesha sehemu ya fedha
aliyopewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa au
huduma au kuzuia sehemu ya fedha iliyopaswa
kwenda kwa mzabuni kwa ajili ya ununuzi wa
bidhaa au huduma.
Mapendekezo hayo yameendelea kuitaka ofisi
husika ya umma ndani ya siku saba baada ya
kutangaza kuwa mzabuni huyo, hafai kupewa
zabuni inayogharimiwa na fedha za umma,
kuwasilisha jina la mzabuni na wakurugenzi wake
kwa mamlaka inayotajwa na sheria husika.
Mamlaka hiyo nayo imetakiwa na mapendekezo
hayo ya sheria, kwamba baada ya kupata taarifa
hiyo, kumfungia mtu au mzabuni husika asipate
zabuni yoyote inayogharimiwa kwa fedha za
umma, kwa muda usiopungua miaka 10.
Sifa za CEO
Katika mapendekezo kwenye Kifungu cha 23 cha
Sheria hiyo, Kifungu Kidogo cha II,
kimezungumzia uteuzi wa maofisa watendaji
wakuu wa ofisi hizo za serikali.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa ofisa mtendaji
mkuu, atateuliwa kutoka kati ya wataalamu
wenye uzoefu wa angalau miaka 10 katika fani
za uhandisi, usanifu wa majengo, sheria,
menejimenti ya ununuzi na usambazaji na
ukadiriaji majengo.
Fani nyingine zilizotajwa ni pamoja na uongozi
wa biashara, mipango ya kiuchumi na maendeleo
au katika fani nyingine yoyote, lakini awe na
uzoefu usio na shaka katika masuala ya ununuzi
wa umma.
Bei ya soko
Katika Kifungu cha Tisa cha Sheria hiyo sehemu
(o) imeitaka ofisi ya umma, wizara au taasisi ya
umma, kila taasisi imetakiwa kuwa na taarifa ya
bei ya soko ya bidhaa na huduma inayotumika
mara kwa mara na ofisi husika kutoka katika ofisi
husika ya umma ili kuhakikisha bei ya bidhaa na
huduma zitakazonunuliwa, zinalingana na za
soko.
Katika kuhakikisha ofisi za umma zinanunua
bidhaa bora kwa bei ya soko, ununuzi wa umma
umetakiwa kwa mujibu wa muswada huo,
kufanyika kwa kuzingatia uaminifu wa hali ya juu,
ushindani, uwajibikaji, kuzingatia kupunguza
gharama, ufanisi, uwazi na kupata thamani ya
fedha iliyotumika.
Aidha, ili kupata bei iliyo chini ya soko bila
kuathiri ubora wa bidhaa au huduma, ofisi husika
kwa nia ya kupata thamani ya fedha na ubora wa
juu, imetakiwa kufanya ununuzi wa bidhaa na
huduma mahususi moja kwa moja kutoka kwa
mtengenezaji, au kiwandani, mwakilishi wa
mtengenezaji au wa kiwanda, muuzaji wa jumla
au mtoa huduma.
Wawekezaji wa ndani
Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka
pale kampuni au taasisi ya umma inapolazimika
kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni
suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya
nchi, ofisi hiyo ya serikali inalazimika kuhakikisha
kuna wataalamu wa ndani ya nchi.
Ushiriki huo wa wataalamu na kampuni za ndani
katika shughuli za ushauri kutoka nje ya nchi,
sheria hiyo imependekeza kuwa, kampuni yoyote
ya ushauri ya nje ya nchi, inapoomba kazi katika
kazi zinazogharimiwa na fedha za umma, lazima
ishirikiane na kampuni, mshauri wa Kitanzania
kwa asilimia mpaka 15.
Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe
zabuni katika shughuli ambazo zinagharimiwa na
fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha
wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia
60 ni Watanzania.
Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi
Watanzania, kampuni husika lazima ieleze
kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa
ndani ya nchi, ambazo itazinunua katika
utekelezaji wa shughuli zake.
Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa na
kupitishwa katika Bunge hili, ili kuzuia matumizi
mabaya ya fedha za umma, ambazo katika bajeti
ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/2016, asilimia
40 ya trilioni 29.53, imepelekwa katika miradi ya
maendeleo.chanzo habar Leo.
0 comments :
Post a Comment