Simu feki yazua kizazaa.soma zaid.
WAKATI kesho Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) ikitarajiwa kutimiza azma yake
ya kuzima simu ‘feki’ za mkononi, upo mtikisiko
na kizaazaa miongoni mwa watumiaji wa vifaa
hivyo vya mawasiliano, wakisaka mbadala na
wengine wakisubiri kuona kama ‘yatatimia’.
Ingawa uzimaji wa simu bandia na kuanza
kutumika kwa teknolojia mpya ya simu za
mkononi kwa Mfumo wa Rajisi, unatarajiwa kuwa
muarobaini wa wizi kwa simu za mkononi na
kiama kwa watukanaji, watumaji picha chafu,
baadhi ya wanajamii wanaipokea hatua hiyo kwa
mtazamo hasi, wakiangalia hasara watakayopata
baada ya simu zao kufungiwa.
Kizaazaa kimekumba siyo tu watumiaji wa simu,
hususan wale ambao wameshabaini kuwa simu
zao ni bandia, bali pia wenye maduka ya simu
ambao baadhi inadaiwa kusafirisha simu hizo
kwenda kuziuza nchi jirani.
Wakati hayo yakijiri miongoni mwa watumiaji wa
simu za mkononi, kwa upande wao, kampuni za
simu za mkononi zimetumia fursa hiyo kufanya
biashara ya simu za mkononi kwa bei nafuu,
itakayowezesha wenye kipato cha chini kumudu
bei yake.
Watamani siku ifike
Baadhi ya wafanyabiashara wa simu jijini Dar es
Salaam waliozungumza na gazeti hili, walieleza
matamanio yao ya kuzimwa simu bandia ili
biashara yao iendelee, kwa kile walichosema
imedorora tangu TCRA ilipotangaza uamuzi wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,
walisema kumekuwa na hofu miongoni mwa
wateja ambao wengi wanachelea kununua simu
kutokana na hofu ya kuuziwa zilizo bandia.
“Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, biashara ya
simu imeyumba kwa kiasi kikubwa kutokana na
tangazo la TCRA,” alisema Mohammed Bakari
ambaye hata hivyo alisema binafsi anauza simu
halali, ambazo pia zimekosa soko kama ilivyo
kawaida kutokana na kuhofia za bandia.
Mfanyabiashara mwingine, Erick Ngamwe
alisema, uamuzi wa serikali wa kuzima simu hizo
ni jambo zuri. Alishauri isitoe muda wa ziada
ambao kwa mujibu wake, utaendelea kuyumbisha
biashara yao.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine wa
Kariakoo, Nassor Said alisema, wapo baadhi yao
ambao wataumia kwa kuwa walikuwa na mzigo
mkubwa wa bidhaa hiyo.
“Hili tunaliona jambo zuri lakini kuna watu
wanaumia, watu walikopa fedha kuagiza mzigo
wa simu leo hii hajamaliza hata kerejesha pesa
yote, simu zinazimwa na anakuwa anapata
hasara, kwahiyo si jambo la kufurahia,” alisema
Said.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliohojiwa juu ya
hatua hiyo inayotarajiwa kutekelezwa kesho,
waliomba muda uongezwe huku walilaumu
kitendo cha mamlaka zinazohusika kufumbia
macho uingizaji wa simu bandia kuwa ni adhabu
kwa watu wenye kipato cha chini.
Wateja wawa makini
Hata hivyo katika maeneo mbalimbali, mwandishi
alishuhudia umakini kwa wanaonunua simu
ambao wengi walikuwa wakilazimika kutumia
kanuni iliyotolewa na TCRA, kubaini kama simu
anayonunua ni bandia au halisi.
Wakiwa kwenye gulio la simu lililoandaliwa na
kampuni za simu jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, walionekana watu wengi waliokuwa
wakinunua simu za gharama nafuu huku wakihoji
maswali kuhusu uhalali wake. Kampuni zatoa ofa
Kampuni zinazotoa huduma za simu zimesema
zinaendelea kusambaza simu za gharama nafuu
nchini na kutoa ushauri kwa wateja .
Alipohojiwa juu ya athari watakazopata wateja
wenye simu feki baada ya simu zao kuzimwa,
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano na
Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosallyn
Mworia alisema laini za wateja hazitaathirika,
bali simu bandia wanazotumika ndizo hazitafanya
kazi.
Wakati huo huo kampuni ya simu ya Airtel
imetangaza ofa kwa watu wanaohitaji simu halali,
kuendana na matakwa ya serikali ya wananchi
wake kutumia simu zinazokubalika kiafya na
zenye ufanisi mkubwa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, kampuni hiyo
imesema Airtel Tanzania imeanzisha ofa ya
kununua kifurushi chenye thamani ya Sh 22,000
kupata simu ya bure.
Mkuu wa kitengo cha Intaneti, Gaurav Dhingra
alisema: “Tunatambua kwamba baadhi ya wateja
wetu bado wanatumia simu ambazo hazina
uhalisia, hivyo wako katika hatari ya kuzimiwa
simu zao hapo itakapofika siku ya Alhamisi, Juni
16 (kesho).”
Wizi wa simu basi
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa
habari na wafanyabiashara wa maduka ya simu
mjini Kigoma jana, Kaimu Meneja wa Kanda ya
Kati wa TCRA, Esuvatie Masinga alisema
teknolojia hiyo itasaidia kudhibiti wizi wa simu za
mkononi nchini.
Alisema simu itakayoibwa na kutolewa taarifa,
itafungwa na haitaweza kutumika mahali popote
duniani. Alisema teknolojia hiyo itadhibiti
matumizi mbalimbali yasiyofaa ya simu za
mkononi, ikiwemo wanaotukana, wanaotuma
picha chafu na matumizi mengine
yanayokatazwa.
Masinga alisema simu inapoibwa, utambulisho wa
simu hiyo utaonekana kwenye laini nyingine
itakayowekwa iwapo simu hiyo itaendelea
kutumika. Mtu aliyekuwa na simu hiyo,
atafuatiliwa na kukamatwa.
Sambamba na hilo, Meneja huyo alisema kuwa
mfumo huo, unatoa faida kwa wanunuzi wa simu,
ambao watapaswa kupewa garantii ya mwaka
mmoja ya matumizi, jambo linalowalazimisha
wafanyabiashara wanaouza simu kuuza simu
halisi na siyo bandia.
Meneja huyo wa TCRA alisema simu zote na
vifaa vyote vya mawasiliano ambavyo ni bandia,
vitazimwa kama ambavyo imeshatangazwa awali
na hakuna muda wa nyongeza kwa simu bandia
kuendelea kutumika.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma, Emanuel Maganga alisema udhibiti wa
Mfumo wa Rajisi wa Simu za Mkononi, utasaidia
kudhibiti uuzwaji wa simu holela, ambao
unachangia kuwafanya wafanyabiashara kukwepa
kukodi.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alishauri bei za simu
iwe ambayo wananchi wote watamudu. Aliomba
mamlaka isimamie hilo, kuhakikisha
linatekelezeka.chanzo habar leo
0 comments :
Post a Comment