Wamiliki wa nyumba Kubanwa.soma zaid.
SERIKALI inatarajia kuwasilisha muswada mpya
wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 bungeni
unaotajwa kuwa utawabana na kuwakamua watu
mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara na
wamiliki wa nyumba.
Muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa kwa
mara ya pili bungeni wiki ijayo, unakuja baada ya
Juni 8, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango,
Dk. Philip Mpango, kusoma bungeni bajeti kuu ya
Serikali ambayo wabunge pamoja na wabobezi
wa masuala ya uchumi walisema itawaumiza
makabwela kutokana na watu wa tabaka la juu
na kati kubanwa.
Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA Jumapili
imezipata kutoka kwa vyanzo vyake mjini
Dodoma jana, zilisema muswada huo
uliowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni Juni
10, mwaka huu na kuwekwa hadharani Juni 13,
unazua hofu hasa kwa wafanyabiashara huku
ukiwataka wenye nyumba kulipa kodi kutoka
katika fedha wanazolipwa na wapangaji wao.
Chanzo kimoja kilisema kuwa katika moja ya
mabadiliko ya vifungu vya muswada huo,
Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) atapitia mkataba wa kodi wa
mwenye nyumba na mpangaji na atatangaza
gharama za upangishaji katika Gazeti la Serikali.
“Rais John Magufuli ameamua kukusanya kodi
katika maeneo ambayo zamani yalikuwa
hayakusanywi na lengo lake ni kuongeza mapato
ya Serikali kupitia vyanzo vipya. Ndiyo maana
kuna muswada unapelekwa bungeni ili sheria za
zamani za fedha zifanyiwe marekebisho,”
kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Marekebisho ya sheria hiyo yatakuwa katika
maeneo mbalimbali na huenda yakabadilisha
kabisa mwenendo wa biashara na shughuli
mbalimbali zinazofanyika hapa nchini.
“Kifungu cha 8 cha sheria kimebadilishwa na
sasa katika muswada huu mpya kitamtaka
Kamishina Mkuu wa TRA kufanya utafiti kuhusu
eneo husika kabla ya kuanza kutoza kodi na kila
eneo litakuwa na gharama zake, hivyo itakuwa ni
vigumu kukwepa au kudanganya.”
Mbali na hayo, pia chanzo kingine kililiambia
MTANZANIA Jumapili kuwa kama mtu atapinga
kadirio la kodi, muswada huo utamtaka alipe
kwanza kwa asilimia 100 ndipo apinge katika
Mahakama ya Kodi.
Kiliendelea kusema kuwa muswada huo
uliosainiwa Mei 26, mwaka huu na Dk. Mpango,
unasema kuna faini ya asilimia tano kwa kila
mwezi kwa mtu atakayechelewa kulipa kodi.
“Kamishina Mkuu wa TRA kapewa mamlaka
makubwa na yenye kuumiza, mathalani muswada
huo utampa mamlaka ya kumlazimisha mtu
kulipa kodi bila kumfikisha mahakamani,”
kilisema.
Pia muswada huo unataka kila kodi au mapato
ya Serikali yatakayokusanywa yapelekwe Serikali
Kuu ili kuyadhibiti yasipotee.
“Kifungu cha 5 cha muswada huo wa sheria ya
fedha kimefanyiwa marekebisho na sasa
kinasema kila kodi au mapato yatakwenda
Serikali Kuu,” kilisema chanzo hicho.
Kwamba muswada huo utamtaka Waziri wa
Fedha baada ya kushauriana na Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) ndipo atoze kodi kutokana na eneo
husika na kutangazwa katika Gazeti la Serikali.
“Muswada huo pia umebadilisha kifungu cha 16
cha sheria ya fedha na kitamtaka Waziri wa
Fedha kushauriana na mwenzake wa Tamisemi
kabla ya kuanza kutoza kodi katika eneo husika,”
kilisema chanzo hicho.
Kiliendelea kusema kuwa baadhi ya wabunge,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Wizara
ya Fedha na Mipango wamekuwa wakikutana na
kufanya vikao vya kuchambua vipengele
mbalimbali vya muswada huo kabla
haujawasilishwa.
Alipotafutwa Dk. Mpango jana ili atoe ufafanuzi
wa vipengele vinavyotajwa kuwa vitakuja
kuwabana wafanyabiashara na kuwakamua
wenye nyumba, simu yake ya mkononi ilikuwa
haipatikani.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Ashatu Kijaji alipotafutwa, hakupokea simu
alipopigiwa na hata alipotumiwa maswali kwa
ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hakujibu, huku
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, pia
simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Akizungumzia muswada huo, mbobezi wa uchumi
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Profesa Haji Semboja, alisema Serikali inapaswa
kutekeleza muswada huo kwa uangalifu ili
kuondoa malalamiko kwa jamii.
Alisema sheria ya kukusanya mapato haina shida
kama inaingiza kipato kwa Serikali kutokana na
nguvu ya mwananchi au chombo kinachopaswa
kukatwa kodi.
“Sidhani kama Serikali hawakuwa na ufahamu na
vipengele vya kodi vinavyotajwa kuwa
vitawaumiza watu, naamini zipo kodi nyingi za
mapato katika ardhi na matumizi ya ardhi, lakini
kama wameamua kudai kodi za wapangaji inabidi
wawe waangalifu.
“Watanzania wengi wenye nyumba ni masikini na
nyumba zipo za aina nyingi kulingana na
thamani, sio kila inayopangishwa inaweza kuwa
na uwezo kulipa kodi,” alisema Profesa Semboja.
Pia alisema malipo ya kodi lazima yaangaliwe na
maeneo husika kwa kufanya utafiti kupitia kwa
wenye nyumba wenyewe.
“Watu wanaangalia nyumba za kupanga, lakini
wanapaswa kujua wapangaji wanaofanya
biashara mfano za fremu wanahangaika hadi
kupata kodi na kusumbua wenye nyumba,
wasiwasi wangu mkubwa kunaweza kukatokea
tatizo la kubambikiziana kodi, kuoneana na kuzua
mianya ya rushwa kwa wakusanya mapato katika
maeneo husika,” alisema.
Profesa Semboja alisema Serikali kupitia TRA
haitakiwi kukurupuka kutekeleza muswada huo
badala yake itoe elimu na taratibu zitakazotumika
ili kuwa na mfumo mzuri wa kukusanya mapato
hayo.
Alisema Serikali inapaswa kuwa na chombo cha
kuangalia na kusimamia faida na hasara
zitokanazo na ukusanyaji wa mapato katika
baadhi ya vyanzo, zikiwemo nyumba za kupanga.
Kuhusu utaratibu wa kila kodi na mapato ya
Serikali kuingia moja kwa moja mfuko wa Serikali
Kuu, alisema wahusika hawapaswi kukurupuka
kuchukua kila kodi kuilekeza huko kwa kuwa
kuna aina nne za kodi ambazo kila moja ina kazi
yake.
“Kuna haja ya kujua tofauti ya kila kodi na
matumizi yake, mfano kuna kodi ambazo
zinapaswa zitolewe ili zisaidie wakazi wa maeneo
husika, sasa kodi za hivyo zikienda serikalini
wananchi watapata wapi huduma zao? Kwa hiyo
hili suala linapaswa liangaliwe kwa undani,
tunajua Serikali inatafuta fedha, lakini umakini
unahitajika,” alisema.
Profesa Semboja alisema inapaswa kutambua
sehemu wanazopaswa kukusanya kodi na
kuzielekeza moja kwa moja serikalini ili
wasiharibu na kuingilia utaratibu wa watu
wengine kukusanya mapato kupitia vyanzo vyao.chanzo mtanzania newspaper.
0 comments :
Post a Comment