Zitto awapiga chenga polisi saa 36.soma zaid.
Zitto Kabwe
* AWATAKA CCM WAMDHIBITI, WAKISHINDWA
WAPINZANI WATAFANYA KAZI HIYO
* AWAPIGA CHENGA POLISI KWA SAA 36,
AHOJIWA NA VYOMBO VYA DOLA DAR
NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kabwe amesema anasikitishwa na Serikali ya
Rais John Magufuli kuwakamata wapinzani, huku
akikitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimdhibiti
haraka.
Zitto ambaye amekuwa akisakwa na Jeshi la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tangu
Jumamosi, alisema kama CCM itashindwa
kumdhibiti Rais Magufuli, basi wapinzani
watatumia njia ya kikatiba kufanya kazi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari makao
makuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana,
Zitto alisema Jeshi la Polisi limepokea maagizo
kutoka ngazi za juu kuwakamata wapinzani
akiwamo yeye.
Alisema anachokifanya Rais Magufuli ni kujenga
mazingira ya kuwa na mtu mmoja
anayezungumza, huku wengine wakidhibitiwa na
vyombo vya dola.
“Sisi hatumwogopi Rais Magufuli kwa sababu
yeye si Mungu, bali ni rais… leo anaweza akawa
rais kesho akaondoka kwenye nafasi hii.
“Natoa salamu maalumu kwa CCM, lazima wawe
na uwezo wa kumdhibiti rais anayetokana na
chama chao, yeye si kiongozi wa chama bali ni
mjumbe wa Kamati Kuu kutokana na nafasi yake
ya urais.
“Viongozi wa chama wakae na kiongozi wao na
wasimwogope kwa sababu kumejengeka tabia ya
wabunge, viongozi wa CCM, viongozi wa Serikali
kumwogopa,” alisema.
Zitto alisema endapo CCM itashindwa kumdhibiti
Rais Magufuli, kuna hatari anaweza kusababisha
wananchi wakakosa imani naye, jambo ambalo
hawatakubali kuliruhusu.
Alisema Serikali imepiga marufuku watu
wasifanye mikutano ya kisiasa wala
makongamano, jambo ambalo kikatiba
halikubaliki hata kidogo.
Zitto alisema wanashindwa kufahamu nini
kinachofichwa na watawala katika bajeti ya
mwaka 2016/17, hadi kufikia Serikali kuogopa
kuzuia watu kutoa mawazo yao.
“Tunalaani vikali juhudi zinazofanywa na Serikali
kuruhusu tabia za kubana wapinzani ambazo
zinajengeka nchini… mambo haya tuliachana nayo
miaka 20 iliyopita…
“Kama wapinzani tunadhibitiwa kiasi hiki, ipo siku
nawaambia Serikali itafanikiwa kudhibiti vyama
vya siasa, itahamia kwenye vyombo vya habari,”
alisema.
Zitto alisema tangu kuanza mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992, hakujawahi kutokea jaribio la
kupindua Serikali tofauti na ilivyokuwa wakati wa
chama kimoja.
Alisema kama Rais Magufuli ataendelea
kuwabana watu wasitoe sauti zao, wanaweza
kutumia njia nyingine kudai haki yao ya kikatiba.
“Endapo hali hiyo itaendelea kuna uwezekano
mkubwa wa Rais Magufuli akaweka rekodi ya
kutawala muhula mmoja, kwa sababu Watanzania
hawatamkubalia kutokana na mwenendo wake.
“Rais anatumia Jeshi la Polisi kudhibiti upinzani,
hatofanikiwa na wanasheria wetu wanajipanga
ndani ya siku mbili kufungua kesi Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam ya kutaka kupata tafsiri
ya haki ya kikatiba ya vyama vya siasa kukutana
na kufanya siasa,” alisema Zitto.
Alisema kumekuwa na dhana miongoni mwa
Watanzania kwamba hata ziara zake alizofanya
nchi jirani huenda kuna mambo kadhaa alijifunza
ikiwamo namna ya kudhibiti upinzani.
“Inawezekana ziara yake ya kwanza nje ya nchi
aliyokwenda Rwanda, ajifunza namna ya kudhibiti
upinzani.
“Tunamwambia Tanzania si Rwanda, bali ni huru
na ya kidemokrasia na itaendelea kuwa hivyo,”
alisema.
KUWINDWA
Akizungumzia kuhusu kusakwa na polisi pamoja
na kuzuiwa kongamano la chama chake kujadili
mapendekezo ya bajeti ya Serikali, Zitto alisema
hadi jana jeshi hilo halijatoa sababu zozote za
kutaka kumkamata.
Alisema anasikitishwa na jeshi hilo kwa
kushindwa kufuata taratibu za kumkamata,
badala yake wamekuwa wakimvizia.
“Hadi sasa polisi hawajatoa sababu ya kunitafuta
na kuzuia kongamano letu, wameendelea
kunivizia tangu Jumamosi hawajafanikiwa.
“Nataka kuwaambia wananchi kuwa nipo salama
kwa siku mbili ambazo natafutwa, vijana wetu wa
usalama wamejitahidi kuhakikisha sikamatwi, hii
ni kuwaonyesha polisi hawawezi kunikamata
wanavyotaka wao, bali kwa kufuata utaratibu
uliopo,” alisema Zitto.
SAA 36 AWAKWEPA POLISI
Chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti kuwa
baada ya kupatikana kwa taarifa za kusakwa kwa
mbunge huyo tangu lilipotangazwa kongamano la
kujadili bajeti lililoandaliwa na chama chake,
alikuwa akisakwa na polisi.
Kilisema kuwa tangu Jumamosi ya wiki iliyopita
Zitto alijikuta akiwakwepa polisi kwa muda wa
saa 36 huku akipita huku na kule kujinusuru na
mkono wa askari hao.
“Zitto baada ya kupata taarifa za kusakwa kwake
aliondoka kwake Jumamosi, na alikwenda hadi
kwa jamaa yake mmoja anayeishi eneo la
Makongo Juu.
“Baada ya dakika chache vijana wa ulinzi wa
ACT-Wazalendo ambao walikuwa wakifuatilia kila
hatua, walimtaka ondoke katika eneo hilo na
alitumia usafiri wa bajaji hadi eneo la Mlimani
City ambako alichukua gari na kwenda Tabata
nyumbani kwa marehemu mama yake.
“Alipofika katika hilo eneo akiwa katika gari
maalumu, walinzi wa ACT-Wazalendo ambao pia
walikuwa wamepiga kambi walimtaka aondoke
kwani kulikuwa na askari waliovaa kiraia ambao
walikuwa wakizunguka katika eneo hilo,” alisema
mtoa habari wetu ambaye hakutaka kutajwa jina
lake.
Kutokana na hali hiyo, Zitto aliondoka na kwenda
Kinyerezi ambako alifuturu huko kwa mmoja wa
rafiki zake na baadae usiku wa manane
alikwenda maeneo ya Kinondoni alikojichimbia
hadi jana alipojitokeza hadharani.
KONGAMANO
Akizungumza jana kuhusu kongamano la kujadili
katiba, Zitto alisema pamoja na kuwapo hali hiyo,
wataendelea na msimamo wao wa kulifanya
katika ofisi za chama chao.
Alisema kongamano hilo litafanyika leo saa 9
mchana na kuwataka wananchi wajitokeze ili
kuijadili bajeti ya Serikali yao.
KAMANDA SIRO
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon
Sirro alikiri jeshi hilo kumsaka Zitto.
Kamanda Sirro alisema Zitto alitakiwa kufika
Kituo cha Kati jana, lakini alikiuka agizo hilo na
kuamua kufanya mkutano na waandishi wa
habari wakati aliagizwa asifanye.
Alisema mwendelezo wa mikutano hiyo, ni dalili
ya kuleta uchochezi ndani yake.
“Zitto tulimkataza asifanye mkutano wowote na
leo (jana) tutampata na tutamkamata tu, na huo
mkutano anaotaka kufanya ofisini kwake ni
marufuku kwa sababu lengo lake ni uchochezi.
“Bila amani hakuna siasa, na siasa inafanyika
kwa sababu amani ipo, kuna makongamano
mengi tunatoa vibali yanafanyika kwa amani, kwa
kawaida polisi tunatoa ulinzi, kwa hili hatutampa
nafasi mtu anayeichafua nchi,” alisema Kamanda
Sirro.
ZITTO POLISI
Ilipofika saa 10:30 jioni jana, MTANZANIA ilipata
taarifa ya kiongozi huyo kuitwa katika Kituo cha
Polisi cha Kati, Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Habari wa
ACT-Wazalendo, Abdallah Khamisi, ilisema polisi
walipiga simu ya kumwita Zitto kupitia kwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi,
Venance Msebo, wakimtaka ahakikishe kiongozi
huyo anafika katika Kituo cha Polisi cha Kati.
Alisema kuwa Zitto alifika kituo cha polisi saa 11
jioni akiwa na viongozi wa chama chake pamoja
na mwanasheria wake Stephen Mwakibola na
kuhojiwa kwa saa moja.
Baada ya mahojiano hayo Zitto aliachiliwa
ambapo alizungumza kwa ufupi kuwa polisi
walikuwa wanamhoji kuhusu kongamano
lililozuiwa na kwamba leo atatoa taarifa zaidi
kuhusu wito huo baada ya kukutana na uongozi
wa chama chake.
WASOMI
Nao wasomi wa kada mbalimbali wamepinga
kitendo cha Jeshi la Polisi kukamata wanasiasa
na kuzuia mikutano ya hadhara kisiasa kwa kudai
kuwa ni ukiukwaji wa katiba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi
hao waliliambia MTANZANIA kuwa kitendo hicho
si tu ni ukiukwaji wa demokrasia, bali pia ni
kuishambulia katiba ya nchi ambayo inaruhusu
demokrasia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine
(SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema
kitendo hicho kinaonyesha Serikali imeamua
kuishambulia katiba moja kwa moja.
Alisema katiba inaruhusu wananchi kukusanyika
na kuwa na uhuru wa kushiriki katika mambo ya
siasa kwa kuwa nchi inaendeshwa na mfumo wa
demokrasia.
“Kuzuia mikutano ya siasa ya hadhara na
kuwakamata baadhi ya wanachama wa vyama
vya upinzani… jambo hili linaanza kuwatia
wasiwasi wananchi,” alisema Profesa Baregu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo
alisema kitendo kilichofanywa na jeshi hilo si
sahihi kwa kuwa siasa ni sehemu ya shughuli za
jamii.
“Kitendo cha kuwakamata wanasiasa wakati
wanafanya shughuli zao za kila siku ni kwenda
kinyume na katiba ya nchi… vyama hivi
vimesajiliwa kisheria na kikatiba na Msajili wa
Vyama vya Siasa anavitambua,” alisema.
Juzi Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilimkamata
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho
(BAVICHA), Patrobas Katambi, Katibu Mkuu wa
Vijana, Julius Mwita, Mbunge wa Tunduma, Frank
Mwakajoka na viongozi wengine wa chama
hicho.chanzo mtanzania
0 comments :
Post a Comment