Kuna msemo usemao mzigo mzito mpe mnyamwezi au msukuma.soma zaid.
VIGOGO mashuhuri wa Chadema waliowahi kuwa
mawaziri wakuu; Edward Lowassa na Frederick
Sumaye, jana waligeuka gumzo ndani ya Mkutano
Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wa kumchagua Rais John Magufuli, kuwa
Mwenyekiti wa tano wa chama hicho.
Gumzo hilo, lilianzishwa na Katibu Mkuu wa
zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alimpomtaka
Askofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat
Gwajima, asimpotoshe Magufuli ili yasije
yakampata ya Sumaye, ambaye sasa anachezea
mchangani Kibaha.
Sumaye mchangani
“Hata akina Sumaye hawakuunda vyama vyao.
Bado wanahangaika; na sasa Sumaye anacheza
mchangani Kibaha,” alisema Makamba.
Sumaye ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa
Kamati Kuu na NEC ya CCM, kwa sasa anawania
uongozi wa Kanda ya Pwani katika Chadema.
Kabla ya kusema kuwa Sumaye anahangaika na
siasa za mchangani, Makamba alimtaka Gwajima
kuacha uongo na kusingizia viongozi wa CCM.
Makamba aliyepewa nafasi ya kumuombea kura
Rais John Magufuli kwa wajumbe wa Mkutano
Mkuu Maalumu wa CCM, alisema anamtia moyo
Magufuli asiogope kuongoza chama, kwani
hataongoza peke yake bali wapo wanachama
wengi watakaomsaidia kazi hiyo.
“Wewe siyo wa kwanza kukataa kazi hii. Hata
watangulizi wako Kikwete na Benjamin Mkapa
nao walifanya hivyo hivyo,“ alisema Makamba
ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC).
Makamba alisema hata manabii na mitume
wengi, kama Haruni, Mussa, Yona au Yunus na
Yeremia walifanya vivyo hivyo, walipopewa
utume au unabii na Mungu, kwani waliogopa
kufanya kazi hizo lakini, alisema mara zote
Mungu aliwaagiza kuwa wasiogope kuwa manabii
na mitume, kwani atatia maneno kwenye vinywa
vyao.
Aidha, Makamba alitaka viongozi wa dini mfano
Askofu Gwajima, waache kumfitini Kikwete eti
kwamba alikuwa hataki kumpa uenyekiti
Magufuli.
“Askofu Gwajima alikuwa anasingizia kuwa
Jakaya kiongozi wetu mpendwa hataki kukupa
uenyekiti. Alikuwa akikuhimiza kuwa kama hataki
uunde chama chako. Huu ni uongo. Gwajima
amemaliza uongo wote,” alisema Makamba na
kumuomba Magufuli asisikilize uongo wa kiongozi
huyo wa kiroho.
Makamba alimtaka Askofu Gwajima atambue
kuwa hata baadhi ya wana-CCM waliojiengua
mwaka jana, hawakuunda vyama vyao badala
yake wameangukia pua.
Aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kumpa kura
zote za ‘Ndiyo’ Rais Magufuli, kisha Makamba
akaanza kutumia uhodari wake wa misemo,
methali, mafumbo na aya za Biblia na Kurani
Tukufu.
“Mzigo wa chama ulikuwa umebebwa na Mkwere
Kikwete ambaye sasa anaondoka; na kwa kuwa
kuna msemo kuwa ‘mzigo mzito mpe Mnyamwezi
au Msukuma, nawaomba wajumbe wote sasa
mzigo wa chama tumpe Msukuma Magufuli,”
alisema na kauli yake hiyo ilishangiliwa na
wajumbe.
Lowassa na ufisadi
Akielezea aina ya kiongozi anayetoka CCM na
anayeingia, Makamba alisema kuwa anayetoka,
Kikwete ni mpiganaji wa ufisadi, kwa kuwa
alifikia hatua ya kumtosa rafiki yake Edward
Lowassa, kuwa hafai kuwa Rais kwa kuwa
anatuhumiwa kwa ufisadi.
Alisema kada wa chama hicho anayeingia baada
ya Kikwete, Dk Magufuli yeye ndiye muasisi wa
Mahakama ya Mafisadi, ambayo tayari
imeshaanzishwa kwa Sheria ya Bunge. Kwa
mujibu wa Makamba, Kikwete ni kiongozi
aliyepiga vita umasikini na anapoondoka,
anayeingia Dk Magufuli msimamo wake ni
asiyefanya kazi na asile.
Kumchinja Kobe
Naye mmoja wa vigogo wa Chadema aliyerejea
CCM, Fred Mpendazoe, alikuja na dhana ya
namna ya kumchinja kobe, akifananisha na
utaratibu uliotumika, kukata jina la Lowassa
katika majina 38 ya wagombea urais.
Mpendazoe alisema Kikwete alifanya ‘timing’
sana kushughulikia ufisadi ndani ya chama hicho,
kwa kuwa kati ya makada hao 38 waliokuwa
wakiwania urais, baadhi akiwemo Lowassa
walikuwa na tuhuma za ufisadi na kukatwa kwa
majina yao, kulifanyika kwa wakati sahihi.
Kuachana na nzi
Mpendazoe pia alisema Wasambaa
walimfundisha msemo mmoja kwamba, mtu
akitaka asifuatwe na nzi, anatakiwa atupe mzoga
na kuongeza kuwa, hatua ya wagombea wenye
tuhuma za rushwa kutupwa, CCM ilitupa kibudu.
Kwa mujibu wa Mpendazoe, kuhamia Chadema
kwa Lowassa, kulisababisha chama hicho na
Ukawa waliomuunga mkono, kupoteza ajenda,
kwa kuwa walimpokea mtu waliyezunguka nchi
nzima wakimtuhumu kwa ufisadi tena wakisema
wanao ushahidi.
“Walipompokea Lowassa, nikasema basi mchezo
umekwisha wamepoteza ajenda,” alisema
Mpendazoe huku akishangaa kitendo cha Ukawa
kudai demokrasia imekuwa ikibanwa.
Gia angani
Mpendazoe alisema anashangaa kusikia Magufuli
anabana demokrasia na kuhoji kati ya chama
kilichotangaza nafasi ya urais na kuruhusu
wagombea 38 kugombea, huku mchujo ukifanyika
hadharani na kilichompata mgombea kwenye
chopa (helikopta), ni kipi chenye demokrasia?
Akifafanua zaidi, Mpendazoe alisema Chadema
ilimpata mgombea wake angani ndani ya
helikopta, na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe
alipokwenda katika vikao, akasema chama hicho
kimebadilisha gia angani.
“Nilihoji iweje uamuzi huo ufanyike bila vikao,”
alisema na kuongeza kuwa kilichofanyika kilikuwa
sawa na biashara na kuhoji kwa nini chama
hicho kisisajiliwe Brela (Ofisi ya Msajili wa
Makampuni) ili kufanya biashara.
CCM B
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema
alihoji yeye kuitwa CCM B, baada ya Rais
Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Parole na kusema inakuwaje yeye aliyetoka
katika chama hicho mwaka 1995, apewe jina hilo.
Alisema kama kupewa cheo na Magufuli, ndio
sababu ya kuitwa CCM B, basi hata Mbunge wa
Vunjo, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti Mwenza wa
Ukawa, ni CCM B kwa kuwa aliteuliwa kuwa
Mbunge na Rais Jakaya Kikwete.
Mrema alisema kama kuitwa kwake CCM B ni
kutokana na kutoka ndani ya CCM; basi Lowassa
na Sumaye ni CCM A, kwa kuwa wao wametoka
mwaka jana wakati yeye ametoka tangu 1995.
Haeleweki
Naye Magufuli alisema alimshangaa Rais
mstaafu Benjamini Mkapa, kwa kumteua mtu
mmoja kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10
mfululizo, wakati waliofanyakazi na Waziri Mkuu
huyo, akiwamo yeye waliona kuwa ni mtu
asiyeeleweka. Waziri Mkuu wa Mkapa, alikuwa
Frederick Sumaye.
Kauli hiyo ya Magufuli, ilitanguliwa na ya
Kikwete, ambaye alishangaa kuona mtu aliyewahi
kuwa Waziri Mkuu, sasa anagombea uenyekiti wa
Kanda.
0 comments :
Post a Comment