Breaking News
Loading...

Advert

Tuesday, October 25, 2016

Walimu wanne wasimamishwa kazi kwa tuhuma za kimapenzi na wanafunzi.

WALIMU wanne wa Shule ya Sekondari
Kitumbeine wilayani Longido Mkoa wa Arusha,
wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada
ya kutuhumiwa kujihusisha na mapenzi na
wanafunzi wao.
Akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mrisho Gambo ambaye yupo wilayani humo kwa
ziara ya siku tano ya kukagua maendeleo na
changamoto, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel
Chongolo alisema hivi sasa uchunguzi
unafanyika, kubaini jinsi walimu hao
walivyojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na
wanafunzi wao.
Chongolo alisema uchunguzi utakapokamilika na
ikithibitika, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema pia kuwa kuna changamoto ya mimba
ya utotoni, ambazo baadhi ya wazazi na walezi
wao wamekuwa wakiwaozesha kutokana na
mila.
Alisema serikali inafuatilia wazazi wenye tabia
hiyo ya kuwaozesha watoto kwenye umri mdogo
kwani tatizo hilo lipo kwa asilimia 13 katika jamii
ya wafugaji.
Hata hivyo, alisema mimba za utotoni
zimepungua kutoka sita mwaka 2013 na kufikia
nne ingawa bado kuna changamoto ya
wasichana kuozeshwa kwenye umri mdogo na
wazazi wao.
"Tupo kwenye uchaguzi ili kubaini kama kweli
walimu hao wamehusika na mahusiano ya
kimapenzi na wanafunzi wao au la na endapo
ikithibitika kuhusu hilo hatua kali za kinidhamu
zinafanyika," alisema bila kuwataja majina
wahusika hao.
Aidha, alisema wilaya hiyo pia ina upungufu wa
miundombinu ya madarasa 128, nyumba za
walimu 281, matundu ya vyoo 393 na madawati
1,320 ambapo katika mwaka huu wa fedha
2016/17 wilaya imejitahidi kujenga madarasa 60,
nyumba za walimu saba pamoja na kuongeza
shule za msingi sita ili kupunguza tatizo hilo.
Baada ya Gambo kupokea taarifa hiyo, alishiriki
kupaua bweni la Shule ya Sekondari Longido
lililoungua.
Alitoa rai kwa polisi kufanya doria za mara kwa
mara shuleni ili kudhibiti matatizo ya moto na
kuimarisha usalama wa wanafunzi, pia
wanafunzi kushirikiana kwa pamoja na walimu ili
kuimarisha ulinzi nyakati za masomo ya usiku.
Alisisitiza kuwa serikali inawasaka wale wote
waliohusika na kitendo cha uchomaji moto shule
mbalimbali mkoani humo ili kuwafikisha kwenye
vyombo vya dola.
Alitoa rai kwa viongozi wa vijiji, kuhakikisha
wanashiriki kupanga ulinzi kwenye maeneo yao
ili kudhibiti mambo mbalimbali ya uvunjifu wa
amani ikiwemo suala la moto.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top