Breaking News
Loading...

Advert

Sunday, January 22, 2017

Rais Trump awatia moyo wamarekani.soma zaid

WASHINGTON, Marekani
DONALD Trump ameapishwa kuwa rais wa 45 wa
Marekani. Alivalia suti nyeusi na kufunga tai
nyekundu, huku Rais Mstaafu Barack Obama,
akiwa amevalia suti nyeusi na tai ya rangi ya
bluu. Waling’ara. Ilikuwa siku ya kupewa heshima
zaidi kwa bilionea huyo wa biashara za majengo
na nyinginezo.
Kabla ya kuapishwa Capitol Hall, Rais mteule,
Donald Trump, alikwenda kuhudhuria ibada katika
Kanisa la Mtakatifu John mjini Washington.
Maelfu ya wananchi waliungana na kiongozi
huyo, huku wengine wakiandamana kupinga urais
wake kitendo ambacho kiliwafanya askari
kutumia muda wa ziada kuwazuia.
Marais wastaafu walihudhuria sherehe hizo ikiwa
ni ishara ya umoja wa kitaifa bila kujali itikadi za
vyama vyao. Miongoni mwa waliokuwepo, George
W. Bush, Bill Clinton, Jimmy Carter pamoja na
waziri Dick Cheney na wengineo.
Katika hotuba yake, Trump alisema huu si wakati
wa maneno bali vitendo na kwamba Marekani
inatakiwa kufaidi matunda ya kazi zao na kufufua
viwanda vilivyofilisiwa. Tafsiri iliyopo kwenye
hotuba hiyo inaonyesha wazi kuwa dunia
inakwenda katika mwelekeo mpya.
Katika tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, Trump
alianza kwa kusifu utamaduni wa kisiasa
uliowekwa nchini mwao pamoja na kummwagia
sifa Rais Obama. “Tutakabiliana na changamoto.
Tutakabiliana na nyakati ngumu. Lakini
tutafanikiwa malengo yetu. Kila baada ya miaka
minne, tunakutana hapa, tunatekeleza wajibu na
kukabidhiana madaraka kwa mujibu wa katiba na
kwa amani, tunamshukuru Rais Obama na mkewe
Michelle kwa juhudi zao ili kufanikisha tukio hili.”
Akizungumzia juu ya msimamo wake katika
utawala wa miaka minne ya kwanza, Trump
alisema: “Kimsingi suala si chama gani
kinachoongoza Serikali kwa sasa, bila kujali
Serikali yetu inaongozwa na watu. Januari 20,
2017 itakumbukwa kama siku ambayo wananchi
walichukua madaraka ya kuongoza nchi yao tena.
Wanaume na wanawake waliosahaulika katika
nchi yetu, hawatasahaulika tena.
“Kwa miongo mingi tumevinufaisha viwanda vya
nje kwa gharama za kuua viwanda vyetu.
Tumetuma majeshi yetu kwenye nchi mbalimbali
na kuyadhoofisha; tumetetea mipaka ya mataifa
mengine wakati tumeshindwa kutetea kwetu.
Tumetumia trilioni ya dola kwa masuala ya nje ya
Marekani, wakati miundombinu yetu nchini
imeharibiwa na kupoteza mvuto wake,
“Kuanzia siku ya leo na zijazo, mtazamo mpya
wa Serikali ni kujali mambo yetu. Toka wakati
huu, tutaanza na Marekani kwanza. Kila uamuzi
utakaofanywa katika masuala ya biashara, kodi,
uhamiaji, sera za nje, utakuwa kwa manufaa ya
wafanyakazi na familia za wananchi wa
Marekani.
“Tunapaswa kulinda mipaka yetu inayotumiwa na
nchi nyingi kutengeneza bidhaa zetu, kuibia
kampuni zetu na kupora ajira zetu. Kuyalinda
hayo kutakuwa na manufaa na kuibua nguvu
mpya,” alisema Trump.
Katika hotuba hiyo, Trump alidhihirisha uzalendo
wa hali ya juu baada ya kutamka wazi kuwa kila
taifa litapewa nafasi katika majadiliano na
Marekani lakini kitakachopewa kipaumbele ni
utaifa wa Marekani kwanza kuliko chochote.
Hata hivyo, kabla ya sherehe hizo mamia ya
watu walibeba mabango tangu saa mbili asubuhi
wakitaka kuelekea kwenye eneo la tukio la
Capitol Hall. Miongoni mwa mabango hayo
yalisema: “Make racist, Afraid Again”. Pia
walibomoa majengo mbalimbali na
kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa
wakiripoti na kupiga picha kwenye matukio ya
kabla, wakati na baada ya kuapishwa.
Atoa amri ya kwanza akiwa Rais
Ikiwa ni saa chache tangu kuapishwa kuwa Rais
wa Marekani, Trump ametia saini amri za Serikali
mojawapo ikiwa ni agizo linalolenga kuifuta bima
ya afya iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Barack
Obama maarufu kama Obamacare.
Agizo hilo lenye lengo la kuipunguzia Serikali
mzigo wa kiuchumi, linaziamuru taasisi za
kiserikali kukomesha hatua zitakazoendeleza
bima hiyo inayofadhiliwa na Serikali. Badala yake
linataka taasisi hizo kupunguza, kuchelewesha au
kufutilia mbali gharama za matibabu ambazo
zilishughulikiwa na bima hiyo.
Hatua ambayo itaweka gharama hiyo kwa
Serikali za majimbo na watu binafsi. Bima hiyo
huwawezesha mamilioni ya Wamarekani
wasiojiweza kupata huduma ya afya kwa
gharama nafuu. Kuiondoa kabisa bima hiyo
kutahitaji muswada kupitishwa katika Bunge la
Marekani.
Wasiwasi wa mataifa ya kigeni
Wakati Trump akijinasibu kama bingwa wa
Wamarekani wafanyakazi, kituo cha sera za kodi
ambacho ni kituo kinachotoa ushauri bila kujali
chama, kinakadiria kwamba mapendekezo yake
ya kodi hayataongeza deni la kiasi cha dola
trilioni 7.2 la Serikali ya Marekani katika kipindi
cha miaka 10 ya mwanzo, lakini mapendekezo
hayo yanatarajiwa kuwasaidia tu Wamarekani
matajiri.
Kuchaguliwa kwake kulipokelewa kwa wasiwasi
na wengi duniani kote, kutokana na sera za
kujitenga za mambo ya kigeni.
Katika mahojiano baada ya Trump kuapishwa,
Makamu Kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel,
alisema: “Kile tulichokisikia leo ni matamshi
mazito ya siasa za kizalendo.”
Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto,
alimpongeza Trump kwa kuampishwa, lakini
alitahadharisha kwamba utaifa, masilahi ya
kitaifa na ulinzi wa Mexico ni masuala ya juu
kabisa.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis,
alimtaka Trump kuongozwa na mfumo wa
maadili akisema ni lazima kuwaangalia masikini
na waliotengwa.
Putin amsubiri Trump
Siku moja baada ya kuapishwa Trump, Rais wa
Urusi, Vladimir Putin, yupo tayari kukutana na
kiongozi huyo mpya wa Marekani.
Msemaji wa Serikali ya Urusi, Dmitry Peskov,
amenukuliwa na shirika la habari la nchi hiyo,
TASS akisema hayo siku moja tu baada ya
kuapishwa kwa Trump.
Uhusiano kati ya Marekani na Urusi haujawa
mzuri katika miaka ya hivi karibuni, huku
Marekani chini ya utawala wa rais aliyemaliza
hatamu yake juzi, Barack Obama, ikiilaumu Urusi
kwa kuingilia uchaguzi wake wa Novemba
mwaka jana.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top