Ziara ya Rais yatumbua watatu Kagera.soma zaid
Baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza
watumishi wote wa Manispaa ya Bukoba mkoani
Kagera waliohusika katika ukarabati wa majengo
ya Shule ya Sekondari Omumwani ambayo
yameonekana kutoendana na thamani ya fedha
zilizotumika wachunguzwe, watumishi watatu wa
manispaa hiyo wamesimamishwa kazi.
Watumishi hao walisimamishwa jana na Katibu
Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani,
baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya
maji iliyomo katika majengo ya shule hiyo.
Shule hiyo ilikarabatiwa kuwapa hifadhi ya muda
wanafunzi wa shule za sekondari Ihungo na
Nyakato zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi
lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka
jana.
Baada ya ukaguzi huo, Athumani alimtaka Kaimu
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chibunu
Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika
moja kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa
shughuli hiyo.
Katika maelezo yake, Athuman alisema aligundua
ukarabati uliofanywa ulikuwa chini ya kiwango na
hauendani na thamani ya Sh milioni 119
zilizotolewa na Serikali.
“Kwanini wakurugenzi hampendi kufuatilia miradi
iliyo katika maeneo yenu? Kama mngefuatilia
mapema, mngegundua ubadhilifu uliofanyika hapa
na kuchukua hatua mapema.
“Kwa hiyo, naagiza kuanzia leo Januari 3 (jana),
mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba uwasimamishe
watumishi wote waliohusika ambao ni Mhandisi
Kitengo cha Ujenzi wa Manispaa ya Bukoba,
Andondile Mwakitalu, Mhandisi Msaidizi, Costane
Felix na fundi Charles Kafumu.
“Hawa lazima wasimamishwe ili kupisha uchunguzi
utakaofanyika kwa ajili ya kulinganisha kazi
iliyofanywa na kiasi cha fedha kilichotumika kama
vinaendana.
“Tatizo jingine nililoligundua ni kutokuwapo kwa
usimamizi mzuri wa mradi huo kutoka kwa
watumishi wa manispaa. Hao nao uchunguzi dhidi
yao utafanyika kwa uwazi na ukweli na
hatutamwonea mtu.
“Sitaki kusikia shughuli hii inasimama eti kwa
sababu ya hawa watu wamesimamishwa, fanya
makabidhiano na wale watakaokuwapo.
“Kaimu mkurugenzi hakikisha mnakabidhiana kila
kitu, hata msumari usibaki na uchague watu
wengine wa kuendelea na kazi ya kusimamia mradi
huu ili ukamilike kwa muda uliopangwa,” alisema.
Naye Mhandisi Mwakitalu aliyesimamishwa,
alisema majengo hayo yalikuwa katika hali mbaya
na kwamba ukarabati wake unahitaji fedha nyingi
ili yarudi katika hali yake ya kawaida.
0 comments :
Post a Comment