KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, ilielezwa jinsi mabilioni ya shilingi yalivyochotwa kwenye akaunti za Shirikisho la Soka (TFF) na kulipwa kwa watendaji wa shirikisho hilo na wadau wengine wa soka kinyume cha taratibu za kiuhasibu. Ilielezwa pia jinsi malipo hayo yalivyofanyika bila wahusika kukatwa kodi ya serikali, kinyume cha Sheria ya Kodi ya Mwaka 2008. Sehemu ya pili ya ripoti hii leo inachimba zaidi jinsi kadhia hiyo ilivyofanywa na watendaji wa TFF... KUHAMIA MJINI Ripoti ya Kampuni ya Ukaguzi ya TAC ambayo ilipewa kazi ya kuwa mkaguzi wa hesabu za shirikisho kwa miaka mitano kuanzia mwaka ulioishia Desemba 31, 2011 inaonyesha zaidi kuwa uongozi wa TFF ulihamishia makao makuu yake Posta jijini Dar es Salaam kutoka Karume jijini bila kufuata taratibu za kibajeti na kimanunuzi na hivyo kulisababishia shirikisho hasara ya mamilioni ya shilingi. Ripoti ya ukaguzi wa TAC inaonyesha shirikisho lililipa Dola 14,580 (Sh. milioni 42.458) mwaka 2014, sawa na Dola 1,215 kwa mwezi, ikiwa ni gharama ya Dola 16 kwa kila mita mraba ya malipo ya pango, umeme, maegesho ya magari ya maofisa na watendaji wake kwenye jengo la Mfuko wa Pensheni wa PSPF lililopo Posta. Inaelezwa kwenye ripoti hiyo kuwa PSPF walipewa zabuni hiyo bila ushindani na uamuzi huo haukuwamo kwenye Mpango wa Manunuzi wa TFF wa Mwaka 2014 na hivyo haukutengewa fungu kwenye bajeti ya shirikisho mwaka huo. "TFF haikuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2011 wakati inatoa zabuni kwa mpangishaji (PSPF). Hatua hii huenda imesababisha kutolewa kwa zabuni kwa mtoa huduma ambaye tozo zake ni kubwa kulinganisha na malipo ya kila mita mraba yaliyoidhinishwa," inaeleza ripoti hiyo. Rais wa TFF (Malinzi), mara tu baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Leodgar Tenga Novemba 2, 2013, alitangaza kuzihamishia Posta ofisi za makao makuu ya TFF. Hata hivyo, ujumbe wa FIFA uliotua nchini Agosti 2014 ukiongozwa na Meneja Miradi (Programu za Afrika), Zelkifli Ngoufonja, ulieleza kutofurahishwa na uamuzi huo na kuuagiza uongozi wa TFF kurejea kwenye majengo ya makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Karume jijini. MALIPO YENYE SHAKA TFF pia imebainika kufanya malipo ambayo si tu kwamba yanatia shaka, bali pia hayana nyaraka za kuthibitisha uhalali wake. Ripoti ya TAC inaeleza kuwa timu ya ukaguzi ilibaini malipo ya aina hiyo kwa Evarist Majuto Maganga aliyepewa na TFF hundi namba 000185 Julai 17, 2014 kwa madai ya kutoa huduma ya Sh. milioni 48.525 kwa shirikisho hilo. Aidha, Innocent Melleck Shirima alilipwa Sh. milioni 3.143 kupitia hundi namba 000036 Februari 6, 2014 kwa kuandaa mkutano wa waandishi wa habari (press conference) kuadhimisha siku 100 za uongozi mpya (wa Malinzi) madarakani. Pia kuna malipo ya Dola za Marekani 51,043 (sawa Sh. milioni 112.55) yaliyofanywa na TFF kupitia hundi namba 239160 (USD 35,280) na 239206 (USD 15,763) kugharamia tiketi za ndege ambazo waliozitumia hawajatajwa kwenye ripoti, hata hivyo. "Tunapendekeza kwamba, katika siku zijazo, malipo yafanyike kwa kuzingatia uwapo wa nyaraka za uthibitisho wa malipo na ankara za madai ya kodi (Tax invoices)," inaeleza zaidi ripoti hiyo. UKWEPAJI KODI TFF pia imebainika kutokata Kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE) ilipomlipa Dola za Marekani 90,000 (Sh. milioni 189) aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen iliyemtimua mwaka 2014. Kutokatwa kwa kodi ya PAYE katika malipo hayo ya fidia ya kuvunjwa kwa mkataba, kulikuwa kinyume cha Ibara ya 59 ya Sheria ya Kodi ya Mwaka 2008 inayowataka waajiri kuwakata kodi hiyo wafanyakazi wao na kuiwasilisha kwenye Mamlaka ya Mapato (TRA). Wakati malipo kwa kocha huyo yalipaswa kuwa Sh. milioni 189, ripoti inabainisha kuwa taarifa za fedha za TFF zimechezewa na baadhi ya nyaraka muhimu za kihasibu kufichwa. Malipo ya Sh. milioni 78.814 yalifanyika kupitia vocha namba 1086 na hundi namba 0607 Machi 3, 2014 na mengine ya Sh. milioni 63.68 kupitia vocha namba 1458 na hundi namba 0059 Aprili 16, 2014. Malipo ya jumla ya Sh. milioni 189 hayaonekani kwenye vitabu vya fedha vya TFF, ripoti inasema. Inaeleza zaidi kuwa timu ya ukaguzi ilibaini kodi ya PAYE ya Sh. milioni 42.636 ya mwaka 2013 pamoja na ya mwaka 2015 ambayo ni Sh. milioni 56.588 zilikuwa hazijalipwa kwa TRA na ankara hizo za madai ya kodi hazikuwekwa kwenye vitabu vya fedha vya TFF. Pia Sh. milioni 5.937 ambazo zilipaswa kulipwa na TFF kwa TRA kutokana na makato ya asilimia tano ya huduma mbalimbali zilizotolewa na washirika wa TFF, hazijalipwa kwa TRA na hazijawekwa kwenye taarifa za fedha za shirikisho, ripoti inasema. MIKATABA YA MANUNUZI Imebainika pia zabuni yenye thamani ya Sh. milioni 1.963 ilitolewa na TFF kwa Kampuni ya M/S Prime Solutions Ltd kwa ajili ya usambazaji wa tiketi bila kufuata taratibu za utangazaji zabuni. Pia Kampuni ya M/S Yabakoko General Supplies ilipewa na TFF zabuni yenye thamani ya Sh. milioni 40.32, kwa ajili ya vifaa vya ofisini na zabuni zote mbili zilitolewa chini ya utaratibu wa utangazwaji wa zabuni wenye mipaka (Restricted tendering). Hata hivyo, ripoti imebainisha kuwa zabuni hizo hazikupaswa kutolewa chini ya utaratibu huo kwa sababu tatu zilizotolewa na timu ya ukaguzi ikiwamo ya kutokidhi masharti ya Kifungu cha 152(c) cha Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013. Kifungu hicho kinasema zabuni za aina hiyo hutolewa pale panapokuwa na uhitaji wa dharura wa vifaa, kazi au huduma wakati panapokuwa na muda mchache wa taasisi kununua au kutangaza zabuni ya wazi ya kitaifa au kimataifa. Sababu ya pili iliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni kutoingizwa kwa vifaa husika kwenye Mpango wa Mwaka wa Manunuzi, jambo ambalo linaonyesha kulikuwa na muda mwingi kwa TFF kupanga njia nyingine ya kufanya manunuzi ya vifaa hivyo. Ripoti hiyo inaeleza kuwa kama TFF walihitaji huduma hiyo, walipaswa kuonyesha nia Januari 2014 ikiwa ni robo ya tatu ya Ligi Kuu na mwezi wa kwanza kiuhasibu. Sababu ya tatu iliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni kwamba, kwa mujibu wa Wakala wa Taifa wa Huduma za Manunuzi, tiketi na vifaa vya ofisini ni matumizi ya kawaida ambayo hayawezi kutangaziwa tenda kwa utaratibu wa utangazwaji wa zabuni wenye mipaka. Kutokana na changamoto ya watendaji wa TFF kutofuata kanuni za manunuzi, jumla ya Sh. milioni 42.313 zilitumika kulipia zabuni hizo mbili ambazo hazijathibitishwa kisheria. UKARABATI WA OFISI Pia imebainika kuwa Septemba 8, 2014, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya M/S Wajenzi Enterprises Building Constractors wenye thamani ya Sh. milioni 70.01 (kabla ya VAT) ili kufanya ukarabati wa ofisi ya shirikisho zilizopo Karume jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, ripoti ya TAC inabainisha kuwa, mkataba huo ambao ulipaswa kutekelezwa kwa miezi mitatu kuanzia Desemba 9, 2014, haukuwa sehemu ya miradi ya bajeti iliyoidhinishwa na TFF mwaka huo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna bodi ya zabuni wala kamati ya zabuni iliyoidhinisha zabuni hiyo. "Kwa kuzingatia ankara za madai ya kodi (Tax Invoice) Na. 0172 za Septemba 12, 2014 kuhusu malipo ya Sh. milioni 70.01, zinaonyesha kulikuwa na malipo ya awali ya Sh. milioni 20 yaliyofanyika awali kabla ya tarehe rasmi ya malipo. Sh. milioni 50.1 zililipwa baadaye," ripoti inaeleza. "Desemba 16, 2014, mzabuni alilipwa kwa fedha taslimu kupitia vocha Na. 001036 ya Desemba 16, 2013 Dola za Marekani 30,000 ambazo zilikuwa sawa na Sh. milioni 51.703 kwa mujibu wa viwango vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) vya kubadilisha fedha ambavyo siku hiyo Dola moja ilikuwa sawa na Sh. 1,734.43. Hivyo, mzabuni alizidishiwa malipo kwa Sh. milioni 1.683." Wakati ukarabati huo ulipaswa kukamilika Machi 9, 2015, ripoti inaeleza kuwa hadi mwishoni mwa Agosti 2015 wakati timu ya ukaguzi ikiwa mbioni kukamilisha ripoti yake, kazi ya ukarabati ilikuwa inaendelea licha ya mradi kudaiwa kukamilika lakini pia haikuonyeshwa nyaraka zozote za kukamilika kwake na za makabidhiano.