RAIS John Magufuli ametoa ubani wa Sh milioni
10 kwa familia za askari wanne waliouawa
katika shambulio la ujambazi Mbande wilayani
Temeke mkoani Dar es Salaaam, huku
akiwataka askari kutokuvunjika moyo katika
utendaji wao wa kazi kutokana na mauaji ya
wenzao, bali walitumie kama kigezo cha
kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, Rais Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali Ernest Mangu na wanafamilia wa
askari wote waliopoteza maisha.
Askari watatu kati ya wanne waliofariki katika
shambulio hilo la Jumanne usiku katika eneo la
benki ya CRDB Mbande, Dar es Salaam ambalo
watu wenye silaha waliwavamia wakiwa kazini
na kuwaua na kupora bunduki mbili aina ya
SMG na risasi 60, waliagwa jana katika Viwanja
vya Polisi Barabara ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo katika
shughuli iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, IGP Mangu
alisema baada ya tukio hilo kutokea,
aliwasiliana na Rais Magufuli ambaye alionesha
kusikitishwa sana na tukio hilo na kumpa pole
yeye, askari pamoja na familia za marehemu.
Miili ya askari walioagwa jana ni Koplo Yahaya
Malima aliyesafirishwa kwenda kuzikwa kijiji cha
Kibuta, wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Tito
Mapunda aliyesafirishwa kwenda kijiji cha
Migoli, wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa na
Gaston Lupanga aliyesafirishwa kwenda mjini
Songea mkoani Ruvuma kwa maziko.
Askari mwingine Koplo Khatib Ame Pandu
alisafirishwa Jumatano jioni kwenda kwao
Zanzibar ambako maziko yalifanyika siku hiyo
hiyo usiku.
Viongozi mbalimbali wa serikali walipata fursa
ya kutoa salamu za rambirambi katika msiba
huo, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda aliamuru wale wote waliofanya uhalifu
huo pamoja na wale wanaofanya vitendo vya
uhalifu jijini Dar es Salaam kushughulikiwa
ipasavyo.
“Katika hili ninaomba wale wa haki za binadamu
wanisamehe, kitendo hiki si cha kuvumilika hata
kidogo kwa kuona wale ambao wamekula kiapo
kutulinda sisi, leo sisi tunakwenda kuwaua wao
halafu tunyamaze, mimi nasema hapa hadharani …
Afande Sirro twanga tu yeyote mtakayekutana
naye msituni,” alisema Makonda.
Makonda alisema kazi ya amani ya vyombo vya
ulinzi ni kubwa hivyo ipo haja ya kuangaliwa
upya kwa taratibu na sheria kuona ni namna
gani askari kama hao wanaopoteza maisha
wakiwa bado vijana wadogo kuwajengea hata
nyumba ili kuwapa faraja wale wanaowaacha
nyuma yao.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro
alisema kitendo walichofanya wahalifu hao kuua
askari ni sawa na kuwasha moto hivyo na wao
watajibu mapigo na kuhakikisha wahalifu hao
wanapatikana.
“Wameuwasha moto na sisi tutauwasha moto
kwelikweli na katika hili tutaomba watu wa Tume
za Haki za Binadamu kutosimama upande
wowote,” alisema Sirro.
Aidha, Waziri Mwigulu aliagiza Jeshi la Polisi
kuendelea bila kukoma kuwasaka majambazi na
wahalifu wote na kuhakikisha wanakamata
waliofanya tukio hilo.
Mwigulu pia ameagiza viongozi wa Jeshi la
Polisi kwa kushirikiana na wizara yake kuangalia
upya sheria na kuona namna bora ya
kuwasaidia askari kuwa na bima za maisha,
huku akiwataka kuhakikisha wanaharakisha
mafao kwa familia za marehemu yanaandaliwa
mapema.
“Mara nyingi kumekuwa na tabia ya usumbufu
kwa ndugu na jamaa za wafiwa kusumbuliwa na
maandalizi ya mirathi kuchukua muda mrefu na
wakati mwingine tukio kama hili tumeshuhudia
wote lilivyotokea na askari wetu kufa wakiwa
kazini lakini bado itaundwa tume kuchunguza ili
mafao yalipwe kwa wafiwa,” alisema Mwigulu.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju alisema kitendo cha kushambulia askari
na kuwaua ni kuichokoza mamlaka ya nchi na
kulaani wote walioshabikia mauaji hayo kwa
namna yeyote ile.
“Kitendo hiki si cha kushabikia na tuache kabisa
kushabikia vitendo vya uvunjifu wa sheria, lakini
pia tutambue kuwa sheria au Katiba ya Nchi haina
mjadala,” alieleza Masaju.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga
alilaani na kupinga mauaji ya kikatili na kusema
kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na haki
ya kuishi ya kila mtu ipo ndani ya Katiba.
Mbali na Mwigulu, viongozi wengine wa serikali
waliotoa heshima za mwisho kwa miili ya
marehemu ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk
Harison Mwakyembe, Masaju, Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf
Masauni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira.
Pia IGP Mangu, Makonda, Mkuu wa Wilaya ya
Temeke, Felix Lyaniva, Meya wa Manispaa ya
Temeke, Abdallah Chaurembo, Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, Mkuu wa
Makosa ya Jinai, DCI, Diwani Athuman pamoja
na makamishna mbalimbali wa Polisi, mahakimu
na wanasheria.
Katika hatua nyingine, mmoja wa majeruhi
katika tukio hilo, Said Ally (36) aliyelazwa katika
Hospitali ya Temeke, amefanyiwa upasuaji na
kutolewa risasi aliyopigwa.
Ally ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la
Mbande Magengeni karibu na benki ya CRDB
ambako tukio hilo lilitokea, alijeruhiwa kwa risasi
hiyo wakati alipotoka nje ya duka lake kuangalia
kuna nini baada ya kusikia milio ya risasi.
Akizungumzia hali ya Ally, Ofisa Habari wa
Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema
kwa mujibu wa taarifa alizopewa na madaktari
ni kwamba majeruhi huyo alifanyiwa upasuaji
huo jana.
“Taarifa nilizopewa ni kwamba amefanyiwa
upasuaji leo (jana) na ametolewa risasi ambayo
ilikuwa mguuni kwake pamoja na ganda la risasi,
lakini anaendelea vizuri,” alisema Msumba.
Majeruhi mwingine ni Azizi Ally aliyekuwa akiuza
chipsi katika mgahawa jirani na benki hiyo,
alijeruhiwa na risasi mkono wake wa kushoto
wakati akikimbia kuokoa uhai wake.
Azizi ambaye alishonwa nyuzi sita katika mkono
huo, alisema anaendelea vizuri kwa kuwa
alipata matibabu muda mfupi baada ya tukio
hilo na aliruhusiwa kurejea nyumbani.