CHADEMA na Chama cha ACT– Wazalendo,
vimejibu tuhuma zilizotolewa na Msemaji wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole
Sendeka.
Juzi Sendeka, alimtuhumu kwa kumshambulia
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
kutokana na misimamo yao ya kukosoa
mwenendo wa utawala wa Rais Dk. John
Magufuli.
Kauli za kumjibu Sendeka zilitolewa kwa nyakati
tofauti jana na vyama hivyo, vilipozungumza na
waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Dar
es Salaam.
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT-
Wazalendo, Habibu Mchange, akimjibu Sendeka,
aliviomba vyombo vya uchunguzi nchini
kuchunguza akaunti, mali na madeni ya Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini ili
kupima kama yanaendana na maisha anayoishi.
Alisema wanavitaka vyombo hivyo kuanza mara
moja kazi ya uchunguzi kwa kuwa wanaamini
Zitto ni mmoja wa viongozi ambaye mali, madeni,
masilahi na akaunti zake viko wazi.
“Ikumbukwe kuwa katiba na kanuni za chama
chetu huwataka viongozi wote wa chama kuweka
hadharani tamko la mali zao na madeni, Zitto
alitekeleza matakwa hayo kisheria, mali pamoja
na madeni yake yako hadharani na mtandaoni.
Tunatambua chama tawala kinaweweseka,
tunataka kiondokane na ugonjwa huo, badala
yake wachukue hatua za uchunguzi dhidi ya
Zitto,” alisema Mchange.
Pia alimgeuzia kibao Sendeka kwa kumtaka
kumkumbusha Rais Magufuli kuweka hadharani
nyaraka zake za mshahara.
“Ole Sendeka amuulize mwenyekiti wake wa
CCM ambaye ni Rais Magufuli kama bado yuko
likizo. Alipokuwa Chato likizo, alipiga simu redio
moja akasema akirudi ataweka ‘salary slips’ wazi,
sasa bado yuko likizo? Tunapiga marufuku
kumhusisha Zitto na siasa nyepesi,” alisema
Mchange.
Akizungumzia kauli kwamba Zitto alikuwa
akiwalinda maswahiba zake alipokuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Mchange alisema anashangazwa
na kauli hiyo kwa kuwa Rais Magufuli amekuwa
akipambana na ufisadi, lakini alishindwa
kumchukulia hatua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu
wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau na badala yake
akamteua kuwa balozi nchini Malaysia.
Mchange alisema katika Ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
Profesa Mussa Assad, kupitia taarifa husika
alitoa hati safi kwa NSSF kwa hesabu za mwaka
wa fedha wa 2014/2015 na hata katika barua ya
mkaguzi kwenda kwa kiongozi wa NSSF,
inaonyesha kuwa halijanunua ardhi yoyote
Kigamboni bali liliingia ubia wa ardhi kwa hisa
(Land for Equity).
“Sijui msemaji wa CCM anatumia taarifa ipi ya
CAG kusema kuwa NSSF ilinunua ardhi kwa bei
ya shilingi milioni 800 aliyomhusisha nayo
kiongozi wetu. Sasa Mkurugenzi wa NSSF
anayesema kapewa ubalozi, ukiangalia
Mwenyekiti wa CCM anapambana na ufisadi,
anamshindwa nini huyo? Ina maana anateua
mafisadi kuwa balozi? Hivyo ni vizuri akieleza
kwa undani ufisadi anaousema kwa kunukuu
ripoti ya CAG kaitoa ukurasa namba ngapi,”
alisema Mchange.
CHADEMA
Naye Mkuu wa Idara ya Uenezi wa Chadema,
Hemed Ali, alimshambulia Sendeka akisema ni
sawa na mtumishi hewa kwa kuwa cheo chake
hakipo kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya CCM na
wala hakipo katika ngazi za utawala Makao
Makuu ya chama hicho.
Hemed alisema hata taarifa aliyoitoa Sendeka
ilikosa mtiririko wa kiuandishi na kimantiki,
kuanzia utangulizi, ujumbe na hitimisho alivyodai
havina uwiano.
Alisema hatua hiyo inatokana na kuwapa nafasi
watu wasio na uwezo na kwamba hata kada
mwenzake, Profesa Sospeter Muhongo, aliwahi
kutahadharisha juu ya uongo wa Sendeka pamoja
na kufeli masomo yake ya kidato cha sita kwa
kupata daraja sifuri.
“Ole Sendeka anaendeleza mwendelezo wa Rais
Dk. Magufuli wa kutokutaka kukosolewa na
wataalamu, wanahabari na Watanzania kwa
ujumla, wakisahau Katiba ya Jamhuri inawapa
Watanzania uhuru wa kutoa maoni,” alisema
Hemed.
Pia alisema hawashangai Sendeka kushambulia
vyombo vya habari kwa kuwa CCM na Rais
Magufuli hawapendi Watanzania watoe maoni, na
ndio maana wanataka kusukuma Muswada wa
Habari.
Akizungumza kuhusu mashambulizi aliyoyatoa
dhidi ya Lowassa, Hemed alisema CCM inaugua
homa yake inayoitwa Lowassaphobia.
“Ndiyo maana kimeacha kuendelea na shughuli
zao na kumwandama Lowassa. Kimsingi
mchakato wa kumpata mgombea urais na
mgombea mwenza wa chama ulikuwa wa
kidemokrasia kwa mujibu wa katiba yetu ambapo
ibara (7.7.16 (a)), kamati kuu inapewa mamlaka
ya kuwafanyia utafiti wagombea urais na
kupeleka ripoti Baraza Kuu,” alisema Hemed.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho
( 7.7. 13 (a)), Baraza Kuu linapendekeza majina
ya wagombea au mgombea aliyejitokeza na
kupitia Ibara ya (7.7.10 (c)), Mkutano Mkuu wa
chama unachagua mgombea urais na mgombea
mwenza.
Alisema Lowassa alipitia hatua zote kama
mwanachama halali wa Chadema kwa mujibu wa
Katiba (5.1) na (5.2).
Pia alikumbushia mchakato wa kumpata
mgombea wa urais kupitia CCM mwaka 2015 kwa
kuuita kuwa haukufuata katiba na kanuni za
chama hicho.
“Nilitarajia Sendeka aeleze kile kiini macho cha
kumchagua Magufuli Dodoma kuwa mgombea
wao, huku wenyewe kwa wenyewe wakipinga
mchakato wa kumpata usiofuata katiba na kanuni
za chama hicho kama walivyojitenga na uamuzi
huo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kutokana
na kutoridhishwa na mwenendo wa uamuzi ndani
ya vikao. Kamati Kuu yao ilipasuka katikati baina
ya wajumbe,” alisema Hemed.
Alisema anakubaliana na Sendeka kuwa
mgombea ni taswira ya chama, lakini alidai kuwa
CCM kwa sasa inaonyesha ni wafinyaji na
wakandamizaji wa demokrasia.
Akijibu tuhuma za kiongozi mmoja wa chama
kupatiwa Dola milioni 15 za Marekani takriban Sh
bilioni 33 za kitanzania, alisema fedha hizo ni
nyingi na zingetosha kuchukua madaraka kamili
kuanzia ngazi ya mtaa hadi urais na si tu
kupanga safu ya ndani ya chama.
“Amesema kuwa yupo kiongozi ndani ya chama
chetu aliyepata dola milioni 15 apange safu ya
uongozi ndani ya chama. Kiuhalisia na kwa
hesabu ndogo tu ni kuwa pesa hiyo si tu
inatosha kupanga uongozi wa ndani, bali ushindi
wa mitaa, kata na halmashauri, ubunge na urais,
hivyo wakati anataja tarakimu hizo ajue na
michanganuo ya hesabu badala ya kuwa
mkurupukaji,” alisema Hemed.chanzo mtanzania