DODOMA
RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), imezidi kuibua namna upigaji
‘dili’ ulivyofanyika kwa fedha za umma katika
taasisi na idara nyeti, zikiwamo Bunge na Ofisi
ya Rais Ikulu.
Katika vitabu 11 vya taarifa ya CAG, imebainika
kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutokana na makisio ya juu, zaidi ya
mahitaji lilinunua samani za Sh milioni 94.344
wakati wa maandalizi ya Bunge Maalumu la
Katiba ambazo sasa hazitumiki.
Hayo yalibainika juzi, baada ya CAG Profesa
Mussa Assad, kukabidhi vitabu vya ukaguzi.
“Wakati wa maandalizi ya Bunge Maalumu la
Katiba, samani zilizonunuliwa zilikuwa zaidi ya
mahitaji, hivyo kusababisha samani zenye
thamani ya Sh milioni 94.344 zimekosa matumizi,
sasa zimehifadhiwa ghalani,” alisema Profesa
Assad.
OFISI YA RAIS IKULU
Ripoti ya CAG pia imefichua namna ambavyo
Ofisi ya Rais Ikulu, ilivyopata hati isiyoridhisha
katika fungu 20, huku Bunge ikitajwa kwenye
fungu 40.
Kwa mujibu wa utaratibu, taarifa hizo kwa undani
hutolewa baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), itapokutana na kuanza
uchambuzi wa kina.
Ripoti hiyo, pia inaonyesha bodi ya mishahara
nayo imepata hati ya aina hiyo.
Licha ya ofisi hizo, Ofisi ya Rais – Baraza la
Mawaziri nayo imepata hati isiyoridhisha pamoja
na ofisi binafsi ya Makamu wa Rais, ofisi binafsi
ya Waziri Mkuu na ofisi ya Rais Utumishi.
Mbali na hilo, pia CAG alisema ofisi ya Makamu
wa Rais nayo imepata hati isiyoridhisha kutokana
na kushindwa kufutilia miradi yenye kipaumbele.
SHULE YA SHERIA
Ripoti hiyo ambayo ukaguzi wake unaishia Juni
30, 2015, pia inaeleza namna Shule Kuu ya
Sheria Tanzania ilivyoingia mkataba wa Sh
milioni 213.561, ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) na Kampuni ya Invention
Technology Limited kwa ajili ya ununuzi wa vifaa
na ufungaji kiungo cha kuwezesha kufanya
mikutano kwa kutumia nyenzo ya runinga.
Hata hivyo, vifaa hivyo vilivyofungwa havijaanza
kufanya kazi kwa sababu hakukuwa na
makubaliano kati ya Shule Kuu ya Sheria na
mahakama ili kuwawezesha wanachuo kufuatilia
mienendo ya kesi kama ilivyokusudiwa.
“Ninashauri Shule Kuu ya Sheria ifuatilie mkataba
huo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa
yanafikiwa kulingana na thamani ya fedha.
“Kitendo cha kushindwa kuweka kiungo husika na
kuwezesha matumizi ya vifaa vilivyonunuliwa,
kunaashiria kutofikiwa kwa thamani ya fedha
kama ilivyokusudiwa,” ilieleza taarifa hiyo.
JICHO APRM
Pia CAG alisema Mpango wa Kujitathimini kwa
Nchi za Afrika (APRM), ulishindwa kuwasilisha
Sh 89,286,386 Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Katika fedha hizo, Sh 61,734,761 zilikuwa kwa
ajili ya mwaka wa fedha 2013/14 na Sh
27,551,625 kwa mwaka wa fedha 2014/15.
“Katika mwaka wa fedha 2014/15, APRM
walipokea Sh 681,221,236 kama ruzuku ya
Serikali. Tunakumbuka APRM ilianzishwa Mei 26,
2004 na Serikali kwa kuridhiwa na Bunge, hadi
wakati wa ukaguzi Desemba Mosi, 2015
sekreterieti ilikuwa inafanya kazi bila kutangazwa
katika gazeti la Serikali, hivyo kukosa hadhi ya
kisheria,” ilieleza taarifa ya CAG.
YALIYOJITOKEZA
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sura ya 10 ilieleza
wakati wa ukaguzi ilibainika kuwa wizara 17,
balozi mbili na sekreterieti za mikoa 11 zilifanya
malipo ya Sh bilioni 11.314 ambayo yalikuwa na
nyaraka pungufu kinyume cha kanuni 86 (1) ya
kanuni za fedha ya mwaka 2001, pia na kanuni
95 (4) na 18 (f) ya kanuni za fedha ya mwaka
2001.
“Nyaraka za viambatanisho zikikosekana inakuwa
vigumu kuthibitisha pasipo shaka uhalali wa
malipo hayo, hivyo kufanya mawanda ya ukaguzi
kuwa finyu,” alisema.
Juzi, Profesa Assad baada ya kusoma ripoti hiyo
aliwakabidhi wenyeviti wa kamati za kudumu za
Bunge; Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Akisema ofisi yake imekagua taasisi za Serikali
Kuu 199, Mamlaka ya Serikali za Mitaa 164 na
mashirika ya umma 102, kati ya 186.
Profesa Assad alisema kwa upande wa miradi ya
maendeleo, ametoa ripoti 799 na kufanya jumla
ya ukaguzi wa fedha.
Akisoma muhtasari wa ripoti kwa zaidi ya saa
mbili, CAG Assad alisema halmashauri zilizopata
hati safi ni 47, hati zenye shaka 113, hati
isiyoridhisha tatu na hati mbaya moja.
Kwa upande wa Serikali Kuu, wizara zilizopata
hati safi ni 180, hati yenye shaka 18,
isiyoridhisha moja na hakuna hati mbaya.
Huku kwa upande wa mashirika ya umma
yaliyopata hati safi ni 99, yenye shaka matatu na
hakuna iliyopata hati isiyoridhisha wala hati
mbaya.