Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Profesa Mussa Assad
By mwandish wetu
Ni tangu Novemba 5, 2014 alipoteuliwe kuwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), akichukua nafasi ya Ludovick Utouh.
Dar es Salaam. Profesa Mussa Assad ni mtu
anayependa kuchangamana na watu, kufanya
mazoezi na kutumia taaluma yake kujiongezea
kipato, lakini hawezi tena kufanya mambo hayo
kadri ya utashi wake.
Ni tangu Novemba 5, 2014 alipoteuliwe kuwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), akichukua nafasi ya Ludovick Utouh.
Katika mahojiano kwa njia ya barua pepe na
Mwananchi, Profesa Assad anasema mambo
hayo ni sehemu ya changamoto anazopambana
nazo tangu aanze kuongoza ofisi hiyo nyeti.
Mbali ya kushindwa kujichanganya na watu,
Profesa Assad amesema kazi aliyopewa
inamnyima fursa ya kutoa ushauri uliokuwa
unamwingizia kipato na amepoteza marafiki wa
zamani japokuwa amepata wapya.
“Nilipoteuliwa kushika nafasi ya CAG na kuwasili
ofisini, nikaambiwa CAG si mtu wa kawaida,
hivyo ilibidi niache baadhi ya mazoea yangu
binafsi suala ambalo si jepesi sana,” anasema
Profesa Assad akijibu swali la Mwananchi
lililotaka kujua changamoto anazokabiliana nazo
tangu alipochaguliwa miaka miwili iliyopita.
“Changamoto kubwa katika masuala binafsi ni
pale ninapotaka kuishi kama Assad na si kama
CAG, jambo ambalo baadaye nimekuja kujifunza
kuwa kwa sasa ni ngumu sana kutekelezeka,”
anasema Profesa Assad na kuongeza:
“Nilizoea kuwa mtu wa kawaida na mwenye
kujichanganya na kila mtu. Nilizoea kutembea
kwa miguu kama sehemu ya mazoezi, lakini sasa
mara nyingi nalazimika kutumia gari ambalo
limenifanya kuongeza uzito mwilini. Hata hivyo,
kuna wakati nakuwa mbishi kidogo. Kwa ajili ya
afya yangu, nalazimika kuliacha gari na
kutembea.”
Kuhusu kuongeza kipato kwa kutumia taaluma
yake, Profesa Assad anasema kimaadili hawezi
kufanya tena kazi za ushauri.
“Kabla sijateuliwa kuwa CAG nilikuwa mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa kawaida
wahadhiri hufanya pia kazi za kutoa ushauri wa
kitaalamu ambao una fedha nyingi tu. Kwa sasa,
kwa mujibu wa dhamana niliyonayo siwezi
kufanya hivyo tena.
“Suala jingine ni kuwa kuna watu wanaposikia
Assad ni CAG, wanakukimbia. Hii ina maana
kwamba unapoteza baadhi ya marafiki zako wa
zamani lakini pia unapata wapya na ndivyo
maisha yalivyo,” anasema.
Profesa Assad (pichani), amezungumzia pia
changamoto za kiofisi akitaja kuwa ni ugumu wa
binadamu kupokea mabadiliko. “Changamoto ya
kwanza niliteuliwa katika kipindi kifupi kabla ya
uchaguzi na kwa kawaida wakati wa uchaguzi
kunakuwa na vuguvugu la mabadiliko na baada
ya uchaguzi kunakuwa na mabadiliko ya uongozi.
“Utendaji wa kazi katika kipindi kama hicho siyo
mwepesi na ni muhimu kufahamu kuwa kazi za
CAG siku zote hutegemewa kuwa nyenzo ya
mabadiliko katika Serikali, taasisi, mashirika ya
umma na nchi kwa jumla,” anasema.
Profesa amebainisha kuwa, binadamu siyo
mwepesi katika kupokea na kukubali mabadiliko.
Anasema utendaji wake hauwezi kufanana na
CAG aliyemtangulia na kwamba, hayo peke yake
ni mabadiliko na hayawezi kupokewa kwa urahisi
ndani na nje ya ofisi.
“Hata hivyo, kwa sasa namshukuru sana
Mwenyezi Mungu kuwa yale mabadiliko ambayo
yalikuwa vigumu kupokewa/kukubalika
yanaendelea kupokewa ndani na nje ya ofisi na
yameanza kuonyesha matunda,” alisema.
Alisema baadhi ya masuala yaliyoanza kuonyesha
mabadiliko ni pamoja na hofu kuhusu utendaji
kazi na mahusiano ya kikazi na kiongozi mpya.
“Kwa sasa watu wameshanielewa na
ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba
tunashirikiana vizuri.”
Alisema suala jingine ni mabadiliko katika
matumizi ya muda wa ofisi. Alisema Serikali ya
Awamu ya Tano imeanzisha mfumo wa utoaji
taarifa za kila siku na kila juma za utendaji wa
kila mtumishi, jambo ambalo halikuwapo.
Suala jingine ni kuhusu mawasiliano, akisema
ukiwa kiongozi lazima ujue kwamba watu
watahitaji kuwasiliana kiofisi na masuala binafsi.
“Siyo jambo jepesi kuwapa fursa hiyo watumishi
wako wote ambao wameenea mikoa yote ya
Tanzania Bara na hata nje ya nchi,” alisema na
kuongeza:
“Ilinilazimu kuanzisha anuani binafsi ya barua
pepe kwa watumishi wa ofisi yangu ili waweze
kunifikia kwa urahisi na mimi kuweza
kuwahudumia kwa wakati. Kwa hili, naweza
kusema ni hatua nzuri iliyotuweka karibu kwa ajili
ya ufanisi wa kazi zetu.”